Na Dunstan Bahai
JUMUIYA ya Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), imesema ipo haja ya kuwepo kwa katiba mpya kama wananchi wanavyohitaji.
Jumuiya hiyo imesema kwamba kutokana na umuhimu huo, imeandaa kongamano
litakalotoa fursa kwa wananchi kuelewa misingi mikuu ya Katiba ya sasa na kutafakari kwa kina haja, maudhui na mchakato wa kupata katiba mpya.
Wakizungumza jana na waandishi wa habari chuoni hapo, viongozi wa UDASA walisema kuwa kama wananchi wa kawaida wameona kuna umuhimu wa kuwepo kwa Katiba mpya, wao watakuwa wa ajabu kama wanataaluma kuwabeza wananchi.
Mwenyekiti wa UDASA Dkt. Mushumbusi Kibogoya, alisema kongamano hilo halitaingilia tume itakayoundwa na Rais ambayo inashughulikia Katiba, bali kuna uwezekano wa kuisaidia.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika kesho kutwa kwenye ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo na litaongozwa na watoa mada Prof. Issa Shivji wa Kigoda cha Mwalimu cha Taaluma za Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) na Jenerali Ulimwengu wa gazeti la Raia Mwema.
Alisema wamelazimika kuwaomba wanataaluma hao kutoa mada kutokana na uzoefu wa muda mrefu wa kupigania demokrasia.
Kwa mujibu wa Dkt. Kibogoya, kogamano hilo si mkutano wa kuandika Katiba mpya, bali ni kwa ajili ya kila mwananchi kuchangia Katiba hiyo iweje na ile ya sasa kuonesha mapungufu yake.“Hatuingilii Tume iliyoundwa na Rais, Rais atabaki kuwa Rais na kama ameunda Tume hiyo kwa lengo la kunyamazisha mijadala ya wananchi, atakuwa amechanganyikiwa.
Tume ni mali ya aliyeiunda, kwa bahati nzuri nchi hii ina historia ya kuunda tume nyingi, lakini tunaamini rais hakuunda tume hiyo kwa lengo la kunyamazisha mijadala ya wananchi.“Tunaamini tume ikimaliza kazi yake, inakabidhi kwa aliyeiunda na mwenye Tume akiona haimfai, anaitupilia mbali,” alisema Dkt. Kibogoya.
Alisema ili kuepuka maelekezo ya wafadhili kwamba waendesheje mijadala hiyo, wamekataa ufadhili wa mtu au taasisi yoyote.“Lazima tuwe makini katika kuendesha mijadala hii na hata wanaoijadili, vinginevyo tutadhani Katiba ya sasa ni mbaya na tukaunda Katiba mbaya zaidi,” alisisitiza.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa UDASA na Mratibu wa Makongamano ya UDASA, Dkt. Kitila Mkumbo, alitoa tahadhari kuwa mwananchi atakeyefika kwenye kongamano hilo asiwe na mtazamo wa kisiasa kwani si lengo la kongamano hilo.Pia alisema wananchi wa kawaida wasiogope kufika kwani kongamano litaendeshwa kwa lugha ya taifa, Kiswahili.
Alisema kongamano hilo litaendeshwa mwaka mzima na wameamua kulianzisha kutokana na kuwepo kwa msigano juu ya mchakato unaofaa kufuatwa katika kufikia katiba mpya.
“Vile vile wananchi wengi wamekuwa wakihoji nini hasa matatizo ya Katiba iliyopo na maudhui gani yawekwe katika Katiba mpya,” alisema.Dkt. Mkumbo alisema pamoja na wananchi wengi kutaka kuwepo kwa katiba mpya, lakini wengi wao hata hii ya sasa hawaijui, hivyo mijadala itasaidia wao kuifahamu na umuhimu wa kufanyiwa mabadiliko kwani haiwezekani hii yote iwe haifai.
Miongoni mwa watu waliopelekewa mialiko ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba, Mwanasheria Mkuu, Makatibu Wakuu wa vyama vya siasa vyenye uwakilishi bungeni na vyama vyote vya kiraia.
No comments:
Post a Comment