13 January 2011

Mabingwa Zambia watua Dar

*Kuzikabili Yanga, Simba

Na Addolph Bruno
MABINGWA wa soka nchini Zambia, timu ya Zesco imetua nchini jana ikiwa na kikosi cha wachezaji 29 kwa ajili kucheza na
Simba na Yanga katika mechi za kimataifa za kirafiki.

Timu hiyo itaanzankucheza na Simba Jumamosi, kabla ya kukutana na Yanga Jumapili katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mechi hizo ni maalumu kwa timu hizo kujiandaa na michuano ya kimataifa ambao Simba itaiwakilisha nchi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika na Yanga itashiriki mashindano CAF.

Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fighton Simkonda alisema michezo hiyo itakuwa kipimo kwa timu yao kujiandaa na Ligi ya Mabingwa.

Alisema timu yake inafahamu vizuri viwango vya timu za Simba na Yanga, hivyo ni nafasi muhimu kwao kucheza kwa kuwa watapata nafasi ya kurekebisha mapungufu yao na kupeana ujuzi.

"Tumewahi kuja Tanzania zaidi ya mara 5 au 6 na tunazifahamu vizuri Simba na Yanga ni timu zenye uwezo katika soka, tumefurahi kupata bahati ya kucheza nao katika kipingi hiki cha kujiandaa na Ligi ya Mabingwa," alisema Kocha huyo.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake nahodha wa ZESCO, Jackob Banda ambaye pia ni mlinda mlango wa timu ya taifa ya Zambia 'Chipolopolo' alisema ni michezo mizuri kwao, ambayo itawapa nafasi ya kubadilisha uzoefu ya soka tofauti na walivyocheza nyumbani kwao kwa muda mrefu.

No comments:

Post a Comment