17 January 2011

Phiri: Wabrazil watatuonesha njia

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri amesema mchezo wao wa kimataifa dhidi ya Atletico Paranaence, kutoka Brazil ndiyo utakaompa hali halisi kuhusu kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.Kauli hiyo imekuja, baada ya timu
yake juzi kupokea kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Zesco ya Zambia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Phiri alisema kufungwa huko kumemfanya agundue kitu miongoni mwa wachezaji wake, kitu ambacho atakifanyia kazi kabla hajakutana na Wabrazili Januari 20, mwaka huu.

"Nimekubali matokeo kwani timu ilicheza chini ya kiwango, lakini nashukuru nimegundua matatizo kadhaa (bila kuyataja) ambayo katika mchezo unaofuata ndiyo utakaotoa picha kamili katika michezo ya Ligi Kuu," alisema Phiri.

Alikiri kuzidiwa katika kipindi cha kwanza kwani wapinzani wao, waliwakamata kila idara lakini anashukuru mabadiliko aliyoyafanya yalileta mabadiliko na hatimaye matokeo kuwa hayo.

Naye Kocha Mkuu wa Zesco FC, Fighton Simukonda akizungumzia mchezo huo ambapo alisema wamekuja nchini kufanya maandalizi kwa ajili ya Klabu Bingwa Afrika, hivyo hawatafanya masihara.

Alisema ndiyo maana wanacheza kwa nguvu na kasi, ili wachezaji wake wajiandae vizuri na watafanya hivyo kwa timu yoyote watakayokutana nayo.

No comments:

Post a Comment