17 January 2011

Treni ya kati kutoanza safari leo

Na Mwandishi Wetu

SAFARI za treni ya kati zilizokuwa zimepangwa kuanza leo zimesogezwa mbele hadi Ijumaa Januari 21, 2011 kutokana na 'kazi ngumu ya kukarabati daraja' lililopo katika stesheni za Bahi na Kintinku.Taarifa ya TRL jana ilisema kuwa
kutokana mkondo wa mto Bububu kuendelea kutririsha maji mengi, kazi hiyo imekuwa ngumu, lakini tathmini za sasa za wahandisi ujenzi na wataalamu wa Reli zinakadiria kazi kazi hiyo kukamilika  Alhamisi.

"Kufuatia makisio hayo mapya ya huduma ya abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma iliyopangwa awali kufanyika Januari 17, 2011 imefutwa na abiria watarejeshewa nauli zao kuanzia Jumatatu Januari 17, 2011 katika stesheni husika walikokatia tiketi za safari," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Uhusiano Kampuni ykwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Hundi Lal Chaudhary, iliongeza kuwa hivi sasa kazi ya ukarabati zinaendelea kwa saa 24, ili lengo la kufungua njia kabla ya Januari 21, 2011 lifikiwe.

Wakati huo huo, haduma maalumu ya usafiri wa abiria wa treni itaondoka Tabora leo jioni kwenda Kigoma na kugeuza Alhamisi saa 11 jioni kurejea Dar es Salaam. Uongozi wa TRL umewataka wadau na wananchi kwa ujumla kuwa na uvumilivu wakati kampuni inafanya kila njia kurejesha huduma zake katika hali ya kawaida.

No comments:

Post a Comment