LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Hispania, Fernando Torres amekana tetesi za kwamba ana mpango wa kuitema Liverpool na badala yake akawataka mashabiki kuwa nyuma ya timu hiyo.Nyota huyo wa Reds, amekuwa
akihusishwa na kuitema klabu hiyo ya Anfield kutokana na mwenendo mbaya msimu huu, ambapo imeshuhudiwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Roy Hodgson akitemwa na nafasi yake kuchukuliwa na kipenzi wa mashabiki wa timu hiyo, Kenny Dalglish.
Kwa kipindi kirefu, mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Atletico Madrid amekuwa akihusishwa na kuhamia kwa wapinzani wao Manchester United, kitu ambacho kwa haraka alikipinga vikali.
Kwa sasa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ana mkataba na klabu hiyo ya Merseys hadi majira ya joto ya mwaka 2013, huku akiwa na uamuzi wa kuongeza mkataba lakini Torres anasema kuwa ataangalia yote hayo mwishoni mwa mkataba.
Hata hivyo Torres, anakiri Reds kucheza chini ya kiwango katika kampeni za mwaka huu na akatoa wito kwa kila mmoja ambaye anaiunga mkono klabu hiyo kuisaidia, ili iweze kurejea kwenye kiwango chake.
"Zaidi ya yote tunahitaji kuungana pamoja," alisema. "Tunapaswa kuishi kwa wakati kwa kila mechi. Tunahitaji kuongeza pointi zaidi, kushinda mechi na kuongeza kiwango chetu kwenye msimamo wa ligi," aliongeza na akasema hiyo ndiyo changamoto kubwa kwao na akaomba mchango mkubwa kutoka kwa mashabiki.
Mchezaji huyo alisema kichwa chake kipo Liverpool na anataka kuisaidia timu hiyo msimu huu, kutokana na kuwa yeye ni mtaalamu na mara zote huwa anaheshimu mkataba.
"Sijawahi kuwazia kuondoka licha ya soka kutegemeana na klabu, Liverpool ilipata mafanikio mengi chini ya Rafa Benitez, jambo ambalo limekuwa gumu kwa kila mmoja kuliiga," alisema Torres
No comments:
Post a Comment