11 January 2011

Ancelotti ahadharisha wachezaji Chelsea

LONDON, England

KOCHA Carlo Ancelotti amewaeleza wachezaji, Chelsea ambao ni mabingwa wa FA Cup kuwa ushindi wa mabao 7-0 iliyoupata katika duru ya tatu ya michuano hiyo dhidi ya Ipswich, hautakuwa na maana kama kiwango hicho hakitahamishiwa
kwenye michuano ya Ligi Kuu ya England.

Mabingwa hao wa England, ambao msimu uliopita walitwaa taji hilo kwa mara ya pili kwa sasa wanashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi hiyo, wakiwa nyuma kwa pointi tisa dhidi ya vinara wa ligi hiyo, Manchester United huku ikiwa imecheza mechi moja zaidi kwa viongozi hao wa ligi.

Mazingira hayo ndiyo yamezua tetesi kuhusu hatma ya kibarua cha kocha Ancelotti, kwenye timu hiyo ya  Stamford Bridge na kwa kuichapa timu hiyo ya Ligi Daraja la Pili, inadiwa matokeo hayo kupokelewa kwa mikono miwili na kocha huyo lakini, Muitaliano huyo anafahamu fika presha itakuja tena endapo watafungwa na wapinzani wao  Blackburn mwishoni mwa wiki.

"Tunahitaji kuwa na aina hii ya uchezaji," alisema. "Matokeo ni mazuri na tumefanya vitu vingi katika mechi hii, ila hatupaswi kujivuna kutokana na kuwa tunahitaji kucheza namna hii katika mechi ijayo dhidi ya Blackburn. Lakini pamoja na ushindi huu kujiamini kwetu kutaongezeka na tutaweza kujianda vyema na mchezo ujao," aliongeza.

Alisema kwa sasa bado wanachelea kusema kwamba kila kitu kipo sawa, japokuwa wana kitu ambacho wamefanya kizuri ila  jambo la msingi ni kwamba walicheza vizuri.

Baada ya mchezo huo Ancelotti, alimpa changamoto mchezaji, Daniel Sturridge kuongeza ushindani dhidi ya chaguo lake la kwanza, Didier Drogba baada ya chipukizi huyo kufunga mabao mawili dhidi ya Ipswich.

Mshambuliaji Sturridge, aliingizwa kwenye kikosi cha kwanza baada ya Drogba kupata majeraha mazoezini siku mbili kabla ya Chelsea, kuanza jitihada zake za kunyakua tena kombe hilo la FA msimu wa tatu mfululizo.

"Kila mchezaji anapasha kuwa tayari wakati muda unapofika," alisema Ancelotti. "Kwa Daniel, amewahi kufunga mabao mengi katika mechi zilizopita akiwa kama mchezaji wa akiba.

"Alistahili kucheza, amecheza vizuri, amefunga mabao ni mchezaji mzuri, mshambuliaji mzuri na hatari," alisema kocha huyo.

Mabao kutoka kwa wachezaji, Salomon Kalou, Nicolas Anelka, mawili kutoka kwa Frank Lampard na bao la kujifunga alilofunga, Carlos Edwards yaliifanya Chelsea kuondoka na ushindi huo mnono dhidi ya timu hiyo isiyo na kocha, Ipswich na ambayo inashika nafasi ya 19 kwenye msimamo wa ligi.

Wachezaji Drogba, Michael Essien, Florent Malouda na Ashley Cole wote waliondolewa katika kikosi cha kwanza kutokana na wasiwasi wa kuwa majeruhi lakini, Ancelotti ana imani watakuwa wamerejea uwanjani lakini ana wasiwasi kuhusu Patrick van Aanholt, ambaye alilazimika kutoka nje ya uwanja dakika ya 20 ya mchezo huo dhidi ya Ipswich, akikabiliwa na matatizo ya nyama za paja.

No comments:

Post a Comment