31 January 2011

Japan yatwaa ubingwa Kombe la Asia

DOHA, Qatar

TIMU ya taifa ya Japan, imeweka rekodi ya kutwaa mara nne kombe la michuano ya Asia, baada ya mshambuliaji wake aliyetokea benchi, Tadanari Lee
kuipatia bao dakika za nyongeza lililoifanya timu hiyo iondoke na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Australia.

Japan ilitwaa taji hilo Jumamosi, baada ya Lee kupachika bao hilo dakika ya 109 kwa shuti la guu la kushoto akiwa umbali wa meta 10, kutoka lango la Australia.

Kabla ya kupatikana bao hilo, Lee  muda wote alikuwa akihaha ndipo baadaye akafanikiwa kuunganisha krosi iliyochongwa na beki wake, Yuto Nagatoma na kuachia mkwaju huo ambao ulimshinda mlinda mlango, Mark Schwarzer.

"Sisi tumecheza michuano mizima kwa ujasiri mkubwa na daima walitaka kulazimisha mchezo wetu," alisema kocha wa Japan Muitaliano, Alberto Zaccheroni. "Tuna timu changa sana," aliongeza.

“Benchi la wachezaji limetoa mchango mkubwa kama, Lee alivyofanya leo,” alisema.

Baada ya mchezo huo, kiungo wa Japan, Keisuka Honda ambaye ni mmoja wa wachezaji ambao walifanya kazi kubwa katika mechi hiyo ya fainali alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Australia kufika hatua hiyo ya fainali, baada ya kujiondoa kwenye michuano ya Oceania na kujiunga na michuano hiyo ya Asia mwaka 2006 na imewahi kufungwa na Japan katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa njia ya penalti miaka minne iliyopita.

No comments:

Post a Comment