Na Peter Mwenda
JAJI Mstaafu Dan Mapigano (72) aliyefariki Jumamosi katika Hospitali ya Aga Khan alizikwa jana katika makaburi ya Kinondoni, Dar es salaam, huku akisifiwa kuwa kutoa hukumu zisizo na utata maisha yake yote.Umati wa
waombelezaji waliofurika kuaga mwili wa marehemu katika Wiwanja vya Mnazi Mmoja wakiongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Bw. Ali Hassan Mwinyi ilielezwa kuwa marehemu Jaji Mapigano wakati wa uhai wake hakuwahi kutoa hukumu yenye utata, jambo linalothibitisha uadilifu wake.
Akitoa salamu za Chama cha Majaji Wastaafu, Mwenyekiti wa chama hicho, Jaji Thomas Mihayo alimweleza Jaji Mapigano kuwa hakuwa mwenye majivuno na kila mara alitoa ushauri kwa majaji wenzake na kuwaasa watende haki kabla ya kutoa hukumu.
"Jaji Mapigano alikuwa safi lakini hakuingilika, alipostaafu hakuacha viporo vya hukumu na hukumu zake aliziandika kwa Kiingereza fasaha," alisema Jaji Mihayo.Alisema Jaji Mapigano hakuona ufahari wa cheo chake na alifarijika kukaa pamoja na wenzake lakini hakuwa tayari kuchangia hoja kabla ya kujua jambo linalozingumziwa.
Alisema Jaji Mapigano hakuwahi kukisaliti kiapo chake alichokula cha kutenda haki katika kazi yake mpaka anakufa, hivyo atakumbukwa na wanasheria wengine nchini.
Chama cha Wanasheria Tanzania Bara nacho kilisema Jaji Mapigano hakuwahi kutoa hukumu yenye utata na katika kipindi chote akiwa Jaji ni hukumu mbili tu zilizowahi kukatiwa rufaa.
Hukumu hizo mbili zilizokatiwa rufani zilitolewa na jopo la majaji watatu akiwemo yeye, lakini hata hivyo hazikushinda.
Katika salamu hizo, Profesa Florance Luoga wa F.K Chambers ambako marehemu alikuwa akifanya kazi ya Uanasheria baada ya kustaafu, qlimtaja kuwa alikuwa mdhibiti mkuu wa sheria katika kampuni hiyo.
"Alipenda kesi zote zinazofika mbele yake, mhusika apate haki halali aliyopaswa kuipata na pengo hilo halitazibika mara moja.
Katika kuaga mwili wa marehemu mawaziri Wakuu wastaafu, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Celine Kombani walihudhuria. Pia walikuwapo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta na Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja.Majaji, wanasheria, mawakili na waombelezaji mengi waliaga mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa katika makaburi ya Kinondoni.
Marehemu Jaji Mapigano alizaliwa mwaka 1939 katika kijiji cha Murangi, katika Wilaya ya Musoma na kusoma Shule ya Msingi Ikizu kabla ya kuchaguliwa kwenda Shule ya Sekondari Bwiru Boys mkoani Mwanza alipomaliza 1956.
Alijiunga na kidato cha tano Tabora Boys alipohitimu mwaka 1959 na kujiunga Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda na kuhitimu shahada wa kwanza ya biashara kabla ya kuhamia masomo ya shahada ya sheria.Mwaka 1966 aliajiriwa na idara ya Mahakama kuwa Hakimu Mkazi na Mwaka 1974 aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Marehemu alistaafu mwaka 1999 na kuanza kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari mwaka 2000 na Jumapili ya Januari 2, alipatwa na kiharusi na kukimbizwa hopitali ya Aga Khan ambako alilazwa chumba cha wagonjwa mahututi na kufariki Januari 15. Mungu ilaze roho ya marehemu mahali pema Pepon. Amen.
Mungu ailaze roho ya marehemu baba yetu Jaji Mapigano,uadilifu aliokuwa nao mzee wetu naomba wadau wa sheria na wanasheria wa leo tuuige. Nawapa pole sana familia ya marehemu, zaidi sana rafiki yangu MAIGA MAPIGANO ambaye tulisoma nae Mazengo High School - Dodoma
ReplyDelete