*Ivory Coats yainyuka 1-0
Na Zahoro Mlanzi
BAO pekee lililofungwa dakika ya 61 na mshambuliaji Kipre Bolou wa Ivory Coast, liliifanya timu hiyo kuondoka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' katika mfululizo wa michezo ya Kombe la Chalenji.Mchezo huo uliopigwa
jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa matokeo hayo kumezifanya timu hizo zilizopo Kundi B mpaka sasa kila moja kuwa na nafasi ya kucheza robo fainali.
Ivory Coast ambayo mchezo wake wa awali ilifungwa mabao 2-1 na Rwanda imefikisha pointi tatu sawa na Zanzibar Heroes huku, Rwanda ikiongoza kundi hilo kwa pointi nne na Sudan inashika mkia ikiwa na pointi moja.
Katika mchezo huo ambao, ulihudhuriwa na maelfu ya mashabiki tofauti na mchezo wa juzi kati ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' na Somalia, ulianza kwa kila timu kumsoma mwenzake.
Lakini kadri muda ulivyosonga mbele ndivyo ulivyobadilika ambapo dakika ya 12, Ali Ahmed Shibori nusura aifungie Zanzibar Heroes bao alipobaki na kipa, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Ivory Coast ilijibu shambulizi hilo dakika 26 kupitia kwa Pipre Tchetche, ambaye akiwa ndani ya eneo la hatari alipiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa Mwadin Ally.
Kipindi cha pili kialinza kwa kasi na Zanzibar Heroes, ikafanya mabadiliko kwa kumtoa Shibori na kuingia Abdi Kassim 'Babi' aliyeleta uhai kwa Zanzibar kutokana na kupeleka mashambulizi ya nguvu.
Wakati Zanzibar Heroes, wakihaha kusaka bao, Ivory Coast walifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 61 lililozaa matunda baada ya Bolou kupiga shuti kali nje ya eneo la hatari lililotinga moja kwa moja wavuni na kumwacha kipa akichupa bila ya mafanikio.
Baada ya kufunga bao hilo, Ivory Coast ilizidisha mashambulizi ambapo dakika ya 79, Bolou nusura aifungie tena timu yake bao la pili baada ya shuti lake kugonga mwamba wa juu na mabeki kuondosha hatari hiyo.
Baada ya mashambulizi hayo, Zanzibar Hereos ilikuja juu na kufanya mashambulizi ya nguvu ambapo zikiwa zimebaki dakika sita kabla ya filimbi ya mwisho kupulizwa, Nadir Haroub alipiga kichwa kilichotoka sentimeta chache golini akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Hamis Mcha.
Katika mchezo wa awali uliopigwa saa nane mchana, timu za Rwanda na Sudan zilitoka suluhu huku Rwanda ikikosa bao la wazi dakika ya 79, baada ya nahodha wake Haruna Niyonzima kupiga shuti lililogonga mwamba na kutoka nje.
No comments:
Post a Comment