02 December 2010

Walinzi Machinga Complex waishiwa uvumilivu

Na David John

WALINZI wanaolinda katika Soko Jipya la Karume wamelalamikia uongozi wa Shilikisho la Machinga Complex kutowalipa mishahara yao takribani miezi mitatu imepita.Walinzi hao ambao waliwakilishwa na mmoja wao ambaye alitinga katika Ofisi za
Majira juzi kutoa malalamiko hayo, alisema wamelazimika kutumia njia hiyo kuwasilisha kilio chao.

"Unajua nimelazimika kufika katika ofisi hizi kwa sababu ya kudai malipo yetu, kazi tunafanya lakini kulipwa hatulipwi, kwanini?" alihoji mfanyakazi huyo huku akiwa katika masikitiko.

Mmoja wa viongozi wa Machinga Complex, Bw. Patrick Joseph alisema ni kweli wanakiri kudaiwa na wafanyakazi hao, lakini tatizo ni pesa lakini hawapendi kudaiwa.

"Ni kweli tunadaiwa, lakini tunaomba wazidi kutuvumilia kwani wao ni muhimu sana katika soko hili, bila wao vitu hivi vitaibwa," alisema.

Alisema walikubaliana kwamba wao kama shirikisho watachukua jukumu la kulipa mishahara hiyo, lakini biashara haiendi kama walivyotarajia, hivyo ni suala la kuvumiliana lakini wana imani watamaliza madeni hayo.

Bw. Joseph alisema anaiomba serikali kuangalia upya juu ya mwenendo mzima wa soko hilo kwani hali ilivyo sasa ni mbaya sana, ni ya kuangalia upya na kufanya jitihada za makusudi kushawishi wafanya biashara kuhamaia katika soko hilo.

No comments:

Post a Comment