Na Elizabeth Mayemba
VIONGOZI wa Simba na Yanga, wameendelea kuhaha ili waweze kuutumia Uwanja wa Taifa au wa Uhuru, katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili.Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu, alisema
tayari viongozi hao wameandika barua Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Wizara ya Michezo ili waruhusiwe kutumia uwanja mmojawapo.
"Viongozi wa pande zote mbili wanahaha kuhangaikia Uwanja wa Taifa na Uhuru, kwa ajili ya mechi za ligi, tunasubiri majibu ya barua hizo," alisema.Alisema wamependekeza Uwanja wa Uhuru kama bado utakuwa haujaanza kufanyiwa ukarabati, wautumie kwanza na kama wataanza kuufanyia ukarabati mapema, wapewe Uwanja wa Taifa.
Sendeu alisema wanapotumia viwanja vya mikoani, hutumia gharama nyingi sana tofauti na wanavyokuwa Dar es Salaam.
Alisema wakiwa wanachezea jijini Dar es Salaam, itakuwa rahisi kwao kujiandaa na michuano ya kimataifa, kuliko kufanya mazoezi mikoani.
Aliongeza kwamba, si kwa timu za Simba na Yanga tu, kucheza Dar es Salaam, pia wanataka mechi zote za ligi zichezwe Uwanja wa Taifa au Uhuru.
No comments:
Post a Comment