15 December 2010

Julio akabidhiwa Serengeti Boys

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA wa zamani wa Klabu ya Simba, Jamhuri Kihwelu,  'Julio',  ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuinoa timu ya Taifa ya vijana wenye miaka chini ya 17 (Serengeti Boys).Kocha huyo baada ya kuondoka Simba, alikwenda
Oman kufundisha soka la kulipwa na baadaye kurudi nchini, sasa ataiongoza timu hiyo katika mashindano ya vijana yatakayofanyika nchini Rwanda,  ambayo Serengeti Boys imealikwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikiho hilo, Sunday Kayuni, alisema wameamua kumteua Julio kutokana na kuamini uwezo wake na kwamba, ataipa mafanikio timu hiyo.

"Mashindano hayo ni kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya vijana ya CECAFA (Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati), yatakayofanyika 2011, michuano hiyo ya Rwanda itawahusisha wenyeji na Kenya," alisema Kayuni.

Mbali na hilo, Kayuni alisema wanatarajia kukutana na klabu 12 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Desemba 18, mwaka huu kwa ajili ya kujadili mashindano ya vijana ya timu zao za umri chini ya miaka 20.

Alisema watajadili ni lini mashindano hayo yafanyike, kutokana na hivi sasa shule nyingi kufungwa, hivyo watakapokutana na viongozi wa klabu watajua nini cha kufanya.

Kayuni alisema, mkoa wowote utakaohitaji kuendesha mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza hatua ya fainali ambayo inashirikisha timu tisa, utatakiwa uwe na zaidi ya sh. milioni 20.

Alisema kama hakutakuwa na mkoa utakaoweza kuendesha mashindano hayo, yana hatihati kutofanyika kwani gharama zake ni kubwa na TFF haina uwezo wa kuyaendesha.

1 comment:

  1. mwenyekiti wa tff jiuzuru,jamhuri kiweru sio kocha,mimi ni mpenzi wa simba,kwa nini timu ya taifa ya vijana msiwachague mohamed msomali,unakumbuka timu mbili za vijana alichagua ndio tukawapata kina mogella,malota,fikili mogoso,costa magoroso na n.k au mansour magraham yule alikuwa kocha wa sigara.mbona huonyeshi kama mpira unaujua.usituletee usomi na uchaga wako ktk soka.munapo omba kuongoza kujuana weka pembeni,fanya mabadiliko ya haraka,kama hufanyi nitakufata nitakwambia uso kwa uso.mimi ukweli unauma

    ReplyDelete