10 December 2010

Wizi mtandao wa benki waibua utata

Na Mnaku Mbani

UTATA unazidi kuongezeka juu ya nani hasa ni wahusika wakuu wa uhalifu wa kupangwa wa fedha kwenye benki za Tanzania, baada ya viongozi wa Umoja wa Mabenki nchini kukanusha vikali
kwamba wafanyakazi wa benki ndio hasa wahusika wa tatizo hilo.

Sekta ya fedha nchini, hasa benki za biashara wamekuwa katika tahadhari kubwa kutokana na kuongezeka kwa uhalifu wa fedha, ambao umesababisha wizi wa mabilioni ya amana za wateja na kuzua hofu juu ya usalama wa fedha zao.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki nchini (TBA) aliyemaliza muda wake, Bw. Ben Christiaanse alisema wafanyakazi wa benki hawawezi kuhusishwa moja kwa moja na wizi huo kwani taarifa zinaonyesha kwamba hakuna hata mfanyakazi mmoja ambaye ameshatiwa hatiani kuhusiana na suala hilo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi wakati wa mkutano mkuu wa 14 wa TBA's, Bw. Christiaanse aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa Benki ya NMB, alisema wahalifu wengi wamekuwa wakitumia udhaifu wa mifumo ya benki katika kufanikisha wizi huo.

Hata hivyo, hatua hii imeelezwa na wachambuzi kuwa benki zilikuwa zikijaribu kunawa mikono juu ya tatizo, kwani kuna baadhi ya wafanyakazi wa benki ambao walikuwa wakijihusisha na uhalifu huo.

Bw. Christiaanse alibainisha kuwa benki zenyewe sasa zinahamasishwa kuwa tayari kukabiliana na tatizo hilo, kuunda kamati za kukabiliana na uhalifu huo ndani ya benki zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Bw. Paschal Kamuzora alikiri juu ya kuongezeka kwa uhalifu huo, akisema suala hilo ni moja ya ajenda za umoja huo yatakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2011.

"Hatupaswi kutumia zimamoto ili kukabiliana na tatizo hili, lakini hatuna haja ya kukaa kimya," alisema Bw. Kamuzora.

Suala hilo pia lilisisitizwa na mwenyekiti mpya wa TBA aliyechaguliwa juzi, Bw. Lawrence Mafuru kuwa uhalifu wa fedha ni moja kati ya masuala ambayo itakuwa katika ajenda ya chama hicho kwa 2011.

3 comments:

  1. Ikiwa mpaka leo wahusika waandamizi wa benki kuu, mabenki, wizara ya fedha na kikosi cha kuzuia rushwa mmeshindwa kuwajua wahalifu, basi NG'ATUKENI na tutafanya kazi wenyewe.

    Nitamshauri JK na bunge liidhinishe fedha kuwatafuta hawa wahalifu kwa bei yoyoye hata kama kuwatumia akina WIKILEAKS!

    Wajibikeni au talivalia njuga suala hili maana hatuna wakati zaidi wa kupoteza!!!

    ReplyDelete
  2. Hawa mabwana wanasahau kwamba sisi wananchi ndio tunaoishi na wafanyakazi wao wa mabenki siku hadi siku, na tunayajua maisha yao kabla na baada ya kuanza wizi huo. Hebu wampe fursa Mh. sana Mbunge Mrema - kikweli kweli arudishe "Tajirika na Mrema" yake alafu uno jinsi wapiga firimbi watavyoibuka na kusanua zali kwa njemba hizo za Benki.

    Wenyewe wakubali tu wamebambikiwa mifumo kanyaboya kwa ajili ya ubahili na kutufanya wote mazuzu. Mfano mdogo tu hizo mashine za ATM, vibosile wa mabenki tena ya umma waliibuka na mitumba ya mashine hizo ambazo tayari zilikuwa na kasoro kwingineko walikoendelea na kutokana na kutokuwa na usalama wa kutosha wakaziondoa zote, sisi tukajiona wajuaji tuje tuzilangulie watanzania. Wajanja walioshtukiwa huko makwao walivyojua zimeishia hapa kwetu wakatuibukia na kujifanya watalii: Wameshakomba mamilioni - na wapumbavu wenye njaa-njaa kama wale walioswekwa ndio wakaharibu dili kiasi fulani, lakini bado hizo takataka za NCA sijui ni uchochoro tosha wa kulambwa fedha za mabenki. Hivi mshajiuliza kulikoni?

    ACHENI hiyo biashara ya kukanusha VIKALI... hata kama mkitimuana kimya kimya dunia hii haina siri, mladi kuna ulaji na binadamu ni mroho na mchoyo, mmoja au wawili baina yenu na wafanyakazi wenu ataona MGAO hautoshi au kwa uroho wake au ule wa wale waliowapunja - WANASEMA AU WATASEMA KULIKONI!

    ReplyDelete
  3. hivi mpaka leo hatuna kitengo cha taifa cha IT cha kuweza kutatua matatizo yahusuyo e-business/e-government? Vyuo vikuu nchini vinahitaji kurasilimali katika sekta hii.

    serikali nayo kwa manufaa ya usalama wa rasilimali za nchi iangalie hili kero.

    ReplyDelete