Na Martha Fataely, Mwanga
MTU mmoja amekufa na mwingine kunusurika baada ya kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha katika milimani wilayani Mwanga usiku wa kuamkia
jana.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Bw. Athumani Mdoe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea Majira ya jioni, na kwamba hakuna nyumba wala mazao ya wananchi yaliyoharibiwa.
Alisema mvua hizo zilikuwa zikinyesha katika maeneo ya minara ya Luami na Chanjale na kuwa maji ya mvua katika wilaya yake yameelekea katika bwawa la Nyumba ya Mungu na Mwanga mjini ambapo kuna makorongo mawili ya Mwanga na Kiruru.
“Hakuna maafa zaidi yaliyojitokeza na hakuna korongo lililokatika, maji hayakutoka nje ya makorongo na yalikuwa na mwendo mkali,” alisema.
Watu walioshuhudia maafa hayo walisema tukio hilo limetokea jana saa mbili usiku katika korongo la Mwanga Mjini wakati mwanamke mmoja, Bi. Mwanamina Soko na mwanawe wa kiume walipokuwa wakivuka korongo hilo na kusombwa na maji.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Bi. Aisha Msangi alisema tukio hilo lilitokea wakati mwanamke huyo akivuka korongo hilo kwenda kituo cha afya cha Mwanga kumuona mgonjwa wao walitumbukia na kusombwa na maji yaliyokuwa yakielekea mto wa Kwamagusha.
“Muda wa jioni hivi, sikumbuki saa tulipata taarifa kwamba huko milimani mvua kubwa zilikuwa zikinyesha …baadaye tukashuka kuona maji yakishuka kwa kasi kupata kwenye mito na mifereji ya hapa mjini,” alisema.
Alisema baadaye walipata taarifa kutoka kwa mtoto wa Bi. Soko (ambaye jina lake halikujulikana mara moja) kuwa walisombwa na mafuriko yeye na mama yake lakini yeye amefanikiwa kujiokoa huku akimwacha mama yake akipelekwa na maji hayo.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Bw. Lucas Ng’hoboko amethibitisha kuwepo kwa tukio la watu hao kusombwa na maji lakini hakuwa na taarifa zaidi juu ya kifo cha mwanamke huyo
No comments:
Post a Comment