10 December 2010

Vijana wanolewa kuchukia rushwa

Na Prosper Mosha

TAASISI isiyo ya kiserikali ya TAYCO inayojihusisha na masuala ya maadili kwa vijana na uongozi bora imetoa mafunzo kwa wanafunzi zaidi ya 200 wa shule za sekondari na vyuo kwa
lengo la kuwaepusha na utoaji na upokeaji wa rushwa.

Mada mbili zilizojadiliwa ni, nafasi ya kijana katika kukuza maadili, utawala bora na uwajibikaji na mchango wa vyombo vya habari katika kukuza maadili, utawala bora na uwajibikaji ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kufikia kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kutoa mafunzo hayo Mkuu wa Uratibu na Utoaji Habari wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Bw. John Kabala alisema kundi la vijana ndilo lililo kwenye hatari ya kujiingiza kwenye vitendo viovu, hivyo ni lazima kuwaepusha na hali hiyo.

Bw. Kabala alisema kuwa siku ya maadili inatakiwa pia kuwafanya watumishi wa idara za umma kutambua wajibu wao kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutotegemea malipo ya ziada, yaani rushwa, baada ya kuwa wamewahudumia na watambue kuwa ni wajibu wao kufanya hivyo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo, Bw. Genus Martin alisema kuwa ipo haja kwa vijana kujitambua kwa nafasi zao ndio maana wamelenga kundi la wanafunzi ambao ndio watendaji na watoa huduma wa baadaye kwa jamii yao inayowazunguka.

No comments:

Post a Comment