08 December 2010

Wanafunzi KCMC wasitisha mgomo

Na Martha Fataely, Moshi

ASKOFU wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Martin Shao ameutaka uongozi wa chuo kishiriki cha Tumaini cha KCMC kuwashirikisha wanafunzi wa chuo hicho katika majadiliano kuhusu kupanda kwa gharama za ada na michango mingine
ambayo yamesababisha mgomo.

Askofu Shao ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya chuo hicho alisema hayo katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dkt.
Ntabaye Moshi kutokana na mgomo wa wanafunzi wa huduma za afya.

Katika taarifa yake hiyo kwa wanafunzi hao, Dkt. Shao aliushauri uongozi wa chuo kujadiliana na wanafunzi kuhusu madai yao ya msingi, yakiwamo ya upungufu wa wahadhiri, miundombinu mibovu, umeme na intaneti na kutoa majibu Desemba 17, mwaka huu.

Alisema wakati juhudi zikiendelea, tayari chuo kimeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwamo ya ununuzi wa transfoma ambayo itafungwa chuoni hapo, huku pia kampuni ya simu nchini TTCL ikianza mchakato wa kufunga intanet kwa miezi mitatu ijayo.

Askofu Shao aliutaka uongozi wa chuo kutafuta wahadhiri wa kudumu ili kuondoa kero kwa wanafunzi hao huku pia wakitakiwa kuchunguza mapungufu yaliyopo katika uongozi wa chuo na kuyatatua.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, Rais wa Serikali ya Wanafunzi, Bw. Desdery Katoto na makamu wake, Bw. Joseph Kitukulu, walisema mgomo umesitishwa lakini madai yao yataendelea kuwapo hadi hapo marekebisho yatakapofanyika.

Walisema wanafunzi hawako tayari kulipa viwango vipya vya ada kwani walishakuwa na mkataba wa kulipa ada ya awali, ambayo pia walishaiwasilisha kwa wafadhili wao na wazazi kwa ajili ya utekelezaji.

Bw. Kitukulu alisema wanafunzi wa mwaka wa pili hadi wa tano wanahitaji kurejeshewa fedha za mahitaji maalumu ya kitivo na malipo ya vitendo, ambapo walilipa kuanzia sh 120,000 hadi 400,000 lakini hawakupata huduma kulingana na fedha zao.

No comments:

Post a Comment