10 December 2010

Ancelotti: Sihofii kibarua changu

LONDON, England

KOCHA wa Chelsea, Carlo Ancelotti amesema ahofii kibarua chake licha ya timu hiyo kushuka kiwango chake katika siku za hivi karibuni.Kikosi hicho cha Stamford Bridge kwa sasa
kimepitwa na vigogo vingine viwili, Arsenal na Manchester United baada ya kupata ushindi mmoja na vipigo katika mechi sita zilizopita kwenye michuano ya Ligi Kuu ya England.

Mtatizo hayo ya ndani yameongezeka hadi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, baada ya vijana hao wa Acelotti ambao tayari wamefuzu hatua ya mtoano ya michuano hiyo ya kundi F kujikuta wakichapwa bao 1-0 na timu ya Marseille.

Licha ya ushindi huo kutokuwa muhimu sana kwao lakini, Ancelotti usiku wa kuamkia jana alichagua kikosi chenye nguvu, ili kuweza kupata ushindi na kupunguza fukuto la kufukuzwa kazi lakini akajikuta akiambulia patupu.

Hata hivyo inaelezwa kuwa mtihani mwingine ambao unaweza kuwa wa mwisho kwa kocha huyo utakuwa ni Jumapili, ambapo timu hiyo itakuwa ikiumana na Tottenham.

"Kila mmoja kwa sasa anafikiria tutafungwa mechi ijayo. Nilitumia kikosi changu imara katika mchezo dhidi ya Marseille kwa sababu kwa sasa tupo katika hali mbaya na huu ndiyo ulikuwa wakati wa kubadilisha hali hiyo," Ancelotti aliwaambia waandishi wa habari.

"Ila tumeikosa nafasi hiyo kwa sababu hatukushinda na hatukucheza vizuri, hivyo hali mbaya kwa sasa inaendelea," aliongeza na akasema kuwa na kwa sasa wanakabiliwa na mechi ngumu, dhidi ya timu nzuri Tottenham ila wamebaki kuwa imara na kuipania mechi hiyo.

Alisema hata hivyo ahofii nafasi yake, japokuwa ni kweli timu yake haifanyi vizuri ila akakiri kuwa wanachopaswa kufanya kwa sasa ni kujitahidi kurejea katika kiwango chao.

Mbali na kutohofia kibarua chake, Ancelotti pia alisononeshwa na kiwango cha mshambuliaji wake, Didier Drogba ambaye timu yake inamtegemea kama shujaa.

Mchezaji huyo wa taifa wa Ivory Coast, ambaye hivi karibuni alikuwa akisumbuliwa na malaria, tangu arejee uwanjani ameshafunga mabao mawili katika mechi 11, huku mabao hayo yakiwa yamepatikana kwa njia ya penalti.

No comments:

Post a Comment