20 December 2010

Watumishi, wanasiasa watakiwa kushirikiana

Na Muhidin Amri, Namtumbo

WATUMISHI wa idara za serikali na viongozi wa vyama vya siasa wametakiwa kushirikiana ili kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo zinazofanywa na wananchi.Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Savery Maketta alipokuwa
akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha kwanza cha Baraza la Madiwani juzi.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa viongozi hasa wa kuchaguliwa na wananchi wanatakiwa kuondoa udhaifu wa usimamizi wa majukumu waliyopewa na wapiga kura ili kuwapunguzia mzigo wa tatatizo ya kila siku.

Aliwataka kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo na kuwa waadilifu na wachapakazi wakubwa kwa ajili ya kumkomboa mwananchi katika lindi la umasikini. Aliwaeleza kwamba wao wamepewa dhamana kubwa na kinachohitajika kwa sasa ni kushirikiana na watumishi wa serikali ngazi ya wilaya hiyo kwa lengo la kufanya kazi za maendeleo.

Pia Bw. Maketta alitumia nafasi hiyo kukanusha taarifa zilizopo wilayani humo kuwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mjini Songea hadi Namtumbo umesitishwa na ahadi ya Rais Jakaya Kikwete ilikuwa ya kuomba kura.

Alisema ujenzi wa barabara hiyo ulisimama kutokana na mkandarasi wake kuagiza mashine maalumu ya kupasulia kokoto ambayo imeshafika eneo la mradi na ujenzi wake unaendelea. Wakati huo huo, Bw. Maketta aliwataka wakazi wa Namtumbo kufaya maandalizi ya kuingiza umeme katika nyumba zao ifikapo Julai mwakani.

Alisema serikali imeshaanza mchakato wa kupeleka nishati hiyo kwa Shirika lake la Umeme (TANESCO) kujiandaa kupeleka nguzo huku mchakato wa kumtafuta mkandarasi atakayepeleka jenereta wilayani huyo ukitarajia kuanza mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment