20 December 2010

Rais Mugabe atishia kulipiza kisasi kwa kampuni za Marekani

HARARE,Zimbabwe

KAMPUNI za Ulaya na Marekani zinazoendesha shughuli  zake nchini Zimbabwe zinakabiliwa na tishio la kuchukuliwa hatua na serikali, iwapo vikwazo vilivyowekwa dhidi ya taifa hilo, havitaondolewa.Vitisho hivyo vimo katika hotuba kali ya
Rais Robert Mugabe aliyoitoa kwenye mkutano wa chama chake cha Zanu PF, mjini Mutare na akasema kwamba wakati umefika kulipiza kisasi dhidi ya Jumuiya  za kimataifa, kwa hatua ambazo zinaumiza watu wake.

Mbali na kutisha kampuni hizo, Rais Mugabe alikwenda mbali akisema kuwa wakati huu ndiyo wa kumaliza Serikali ya pamoja baina ya chama chake na Waziri Mkuu Bw. Morgan Tsvangirai iliyoundwa baada ya kufikiwa makubaliano ya mwaka 2008 na ambayo inatarajiwa kufikia ukingoni mwezi Februari mwaka ujao.

Zaidi ya wajumbe  4,000  wa chama hicho cha Zanu-PF walihudhuria mkutano huo ambao unatarajia kumchagua Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 86 kuwa mgombea wake katika Uchaguzi Mkuu ujao.

"Ni kwanini tuendelee kuwa na kampuni  400 kutoka Uingereza ziendelee kuendesha shughuli zake bure?"alihoji Rais Mugabe."Ni kwa nini tuendelee kuwa na kampuni na taasisi zinazosaidiwa na Uingereza na Marekani bila kuleta faida?sasa ni wakati wa kulipiza kisasi,"aliongeza kiongozi huyo.

Kwa mujibu wa sheria za  Zimbabwe raia wa nchi hiyo wanapaswa kupata asilimia 51 ya biashara za nje na kiongozi huyo anasema kuwa wataenda kutengua  sheria hiyo na endapo vikwazo hivyo vitaendelea basi wataibadili na kuwafanya raia kumiliki asilimia  100 ya biashara hiyo.

Mataifa ya Magharibi yamemuwekea vikwazo vya kusafiri na kiuchumi Rais Mugabe,mkewe na watu wanaomzunguka.Mbali na viongozi hao, pia Zimbabwe na kampuni za nchi hiyo zimewekewa vikwazo vya kibiashara na mataifa hayo ya Magharibi.

Katika hotuba hiyo, Rais  Mugabe vilevile aliuambia mkutano huo kuwa biashara ya Serikali ya muungano kati ya chama chake na chama cha Bw.  Tsvangirai cha  Movement for Democratic Change haiwezi kuruhusiwa ikaendelea.Akizungumza kwa lugha ya kabila lake la Kishona,aliifananisha serikali hiyo ya kitaifa kama ndoa isiyokuwa na furaha ambayo kila mmoja anakuwa na ndoto zake.

"Tulikubaliana kuwa tutafanya kazi pamoja kwa lengo la kumaliza kila kitu kama kuleta amani,utengamano kisiasa lakini kwa sasa kuna wengine wanaanzisha masuala mengine,"alisema.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza  BBC,Bi. Karen Allen,aliripoti kutoka katika mji huo wa Mutare akisema kuwa Rais Mugabe anajaribu kurejesha umaarufu ambao aliupoteza wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika miaka miwili iliyopita.

1 comment:

  1. Hawa ndiyo viongozi tunaowataka katika Afrika. Tumechoka na Ukoloni Mambo leo. Hawa Wazungu walioiwekea vikwazo Zimbabwe halafu bado wanaendelea kuendesha biashara za kifisadi ndani ya nchi hiyo hao walaaniwe kabisa na yafaa wafukuzwe au hiyo! Hayo ndiyo mauaji yafaa miradi yao ichomwe moto yote na wao wenyewe. Hata wanaoinyonya tanzania leo wafukuzwe kabisa lasivyo nao waingie mkumbo huo huo naona serikali ya Kikwete inawaonea aibu basi tunaanza wenye nchi kumwondoa mmoja baada ya mwingine

    ReplyDelete