20 December 2010

Diwani: Wengi hatujawahi kuona katiba

Na Suleiman Abeid, Meatu

WAKATI mjadala wa kuishinikiza mabali ya katiba, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Shinyanga wameomba kupatiwa nakala ya katiba kila mmoja kwa kuwa wengi wao hawaifahamu.Walisema wakipatiwa nakala hiyo
wataweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu.Ombi hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita mara baada ya kuapishwa rasmi kuanza kazi ambapo walisema kwa kipindi kirefu wamekuwa wakifanya shughuli zao bila kuwa na katiba.

“Mheshimiwa mwenyekiti tuna ombi moja la msingi, tunaomba tupatiwe nakala ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maana wengi wetu hapa hatuifahamu, sasa iwapo tutakuwa na katiba ni wazi kuwa tutafanya shughuli zetu kwa uhakika na kwa kuizingatia.

“Ni vigumu kutekeleza suala zima la utawala bora iwapo hatuifahamu katiba yetu. Tunaisikia tu, wengine hatujapata hata kuiona katiba hiyo machoni inafananaje, sasa tutafutiwe katiba na kila diwani apatiwe nakala moja, hata kama ni kwa kuzinunua tupo tayari kufanya hivyo,” alieleza mmoja wa madiwani hao.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, Bi. Upendo Sanga aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo la madiwani na kueleza kuwa ni jambo linalowezekana.“Mheshimiwa mwenyekiti, suala la katiba ni suala muhimu, ni vizuri viongozi wetu wakaongoza kwa kuzingatia katiba ya nchi, bila ya kuwa na katiba, ni wazi kuwa
utekelezaji wa dhana nzima ya utawala bora utakuwa mgumu, naahidi kulifanyia kazi ombi hilo mapema iwezekanavyo,” alieleza Bi. Sanga.

Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Meatu mwishoni mwa wiki liliwachagua Bw. Pius Machungwa kuwa mwenyekiti na Bw. Bassu Kayungilo kuwa makamu wake.

2 comments:

  1. Nawapa pongezi madiwani hawa kwa kuwa wakweli. Wapo watanzania wengi sasa hivi wamedandia boti ya kutaka katiba mpya, lakini ukiwauliza kilichomo kwenye katiba iliyopo, wanaingia mitini.

    Ni wazi kwamba bila kuijua katiba iliyopo, michango yetu kwenye katiba mpya itakuwa finyu sana.

    ReplyDelete
  2. Swala la katiba halifahamiki kwa kila mmoja wa watanzania. Isipokuwa yatokanayo na katiba ndiyo wananchi wanaweza kuyajua.Wanao itumia kama msahafu niwana sheria na baadhi ya wasomi kwani hata katika mitaala ya Tanzania sehemu inayofundisha katiba sikumbuki vizuri kama ni kubwa kwa wahitimu wetu. Hivyo nivizuri busara zitumike katika kufanya mabadiriko ndani yake. Hii ni kwamba chama tawala kwa kutaka kuchelewesha hilo wanaweza kutaka kula ya maoni kutoka kwa wananchi wasiyo ijua mfano mdogo ni huo wa madiwani wa Meatu ambao kimsingi wanapashwa angalau kuijua. Hivyo wataalamu wa katiba, makundi mbali mbali ya jamii yakutane nakuangalia mambo ambayo yanatumiwa na watawala kwamanufaa yao nakuacha taifa katika malalamiko na hasara nyingi za kiuchumi na kijamii. Utakuta wananchi wanalaumu tume ya uchaguzi au mahakama imetoa adhabu ndogo, au mbunge/waziri huyu hatufai kwakuwa katiba hailuhusu kumpigia kula ya imani huwezi kumtoa hadi muda wake upite. Ikumbukwe swala la gharama si lamsingi kwani vitu vingapi taifa linalipia kinyume na maslahi ya taifa mfano ni rada na kampuni ya umeme ambayo tutailipa mabilioni hivi karibuni.

    Ikumbukwe wakati wa vyama vingi vinaanza ukusanyaji wa maoni ulio ongozwa na marehem jaji Nyarari, kwa wananchi ulionyesha asilimia 80% walitaka chama kimoja kimsingi ni juhudi iliyo fanywa na chama tawala kukataa vyama vingi kuwa vina vulugu. Ila busara ya marehemu Mwalimu Nyerere akasema 20% siyo ndogo ndiyo akashauri vyama vingi vikaanza. Ila chama tawala walipokea hilo kwa shingo upande na wonga wa misaada ya nchi za nje. Hivyo katiba mpya ni lazima iweke majibu ya kelo za muda mrefu na taifa liweze kusonga mbele.

    ReplyDelete