Na Rabia Bakari
WASHTAKIWA watatu katika kesi ya wizi wa kutumia silaha wamefanya kioja cha aina yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kuvua nguo kwa sababu zilizodaiwa kuwa ni kupinga hukumu ya kuachiwa huru, kisha kukamatwa tena.Kioja
hicho kilitokea jana mahakamani hapo na kusababisha askari waliokuwepo eneo la mahakama kutumia nguvu ili kuwadhibiti washtakiwa hao ambao licha ya kuvua nguo lakini walionesha dalili za kufanya fujo huku wakipiga kelele.
Askari polisi zaidi ya 10 waliwashika kwa nguvu huku washtakiwa hao wakiendelea kugoma kuvaa nguo ambapo waliwadhibiti kwa kuwafunga pingu na baadaye kuwaburuza wakiwa uchi hadi katika mahabusu ya mahakama hiyo.Washtakiwa hao ambao ni Bw. Samuel Joseph, Bw.Said Zacharia na Bw. Said Idd awali walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika kesi namba 184 ya mwaka 2010.
Hati ya mashtaka ya kesi hiyo ilidai kuwa mnamo Juni 4 mwaka huu majira ya saa 9:00 jioni maeneo ya Mchikichini jijini Dar es Salaam, waliiba vitu mbalimbali zikiwemo simu mbili za mkononi aina ya Samsung na Nokia pamoja na nyaraka mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya Sh.467,000 mali ya Bw. David Mkombozi na kabla ya kufanya wizi huo walidaiwa kumjeruhi mwenye mali kwa kumkatakata kichwani kwa kutumia panga ili waweze kujipatia vitu hivyo kwa urahisi.
Kesi hiyo iliendesha kwa miezi kadhaa na ilipofika jana, saa 6:15 mchana Hakimu Mkazi, Bi. Ritha Tarimo aliwaachia huru washtakiwa hao chini ya kifungu cha 225 (4) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) cha mwaka 1985 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.Kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) ya mwaka 1985, kifungu cha 225 (4) kinaruhusu mshtakiwa kukamatwa tena na askari polisi endapo wataona kuna sababu ya kufanya hivyo na ndivyo ilivyofanyika kwa washtakiwa hao.
Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa awali, na ilifutwa kutokana na Wakili wa serikali, Bw. Leornad Chalo kudai upande wa mashtaka hawakua na jalada la polisi la kesi hiyo. Baada ya washtakiwa hao kuachiwa huru, askari walitanda nje ya mahakama hiyo kwa lengo la kuwakamata, jambo ambalo lililowafanya washtakiwa hao kuvua nguo kupinga kukamatwa tena.
Kufuatia hali hiyo, askari hao walianza kuwalazimisha wavae nguo lakini washtakiwa waligoma huku wakilia na kupiga kelele kwa maelezo kuwa jela kuna hali mbaya.
No comments:
Post a Comment