15 December 2010

Sifanyi biashara ya mbao – Dkt. Chami

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya gazeti hili kuandika habari kuhusu baadhi ya viongozi akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Cyril Chami kupewa vibali vya kuvuna magogo katika msitu wa serikali wa Sao Hill mkoani Iringa, kiongozi huyo amekanusha
taarifa hizo na kubainisha kwamba hafanyi biashara ya mbao kama ilivyodaiwa kwani kibali alichoomba, ni kwa ajili ya kupata mbao za kusaidia ujenzi wa shule zinazoendelea kujengwa jimboni kwake.

Aidha Dkt. Chami amelalamikia taarifa hizo na kubainisha kwamba zilichapishwa kwa nia mbaya ya kupotosha ukweli katika suala hilo na kamwe hazikulenga kujenga bali kubomoa.Katika habari hizo ziliyochapishwa Jumamosi iliyopita zilimtaja, Dkt. Chami na baadhi ya viongozi wenzake wa serikali wakiwemo mawaziri kwamba wanafanya biashara ya kuvuna magogo kwenye msitu wa serikali uliopo Mufindi mkoani Iringa hali iliyozua mvutano kati yao na wavunaji wadogo.

Katika taarifa yake kwa gazeti hili, Dkt. Chami alisema endapo mwandishi wa habari hiyo angefanya utafiti angepata ukweli kuwa hata barua ya kuomba kibali hicho, ilisisitiza kuwa mbao hizo ni kwa ajili ya ujenzi wa shule na si kwa shughuli nyingine yoyote.Dkt. Chami alisema  aliomba kibali hicho mara ya kwanza mwaka jana na akapata lakini kutokana na gharama kubwa za kuvuna na kulipa kodi ya serikali huku uwezo wake ukiwa mdogo, alishindwa kuvuna.

“Pamoja na ukweli kwamba niliomba kibali kwa ajili ya ujenzi wa mashule, kibali kilipotoka kilinitaka nilipie kodi zote za serikali kama walipavyo wafanyabiashara wa mbao na nilipokosa uwezo, niliwaachia wengine wakavuna. Ningekuwa nafanya biashara ya mbao ningechukua mkopo benki kwa sababu najua kwamba ningekuwa na uwezo wa kuurudisha mkopo huo baada ya mauzo ya mbao,” alisema, Dkt. Chami na kuongeza;

“Mwaka huu niliomba tena, na najipanga kutafuta namna ya kuvuna,  mbao nitakazopata, nitazitumia kusaidia shule za sekondari za jimbo langu ambazo ziko katika hatua za awali za ujenzi. Lengo langu si kufanya biashara,” alisisitiza waziri huyo huku akiwataka waandishi wa habari kuwa makini katika utendaji kazi wao kwani bila kufanya hivyo, wanaweza kusababisha migongano isiyo ya lzima ndani ya jamii.

Akaongeza kusema;"Kama mwandishi angekuwa makini angeniuliza kabla ya kukimbilia kuchapisha habari hizo, mimi ningempa maelezo haya ili yampe mwanga katika habari yake."Alisema kwa mtazamo wake, ni vema zaidi msitu wa Serikali wa Sao Hill pamoja na misitu mingine kama hiyo  ikatumika kwanza kutoa mbao za kuihudumia jamii kama katika ujenzi wa shule na zahanati ndipo wafanyabiashara wanaotafuta faida binafsi wapatiwe fursa hiyo.

3 comments:

  1. WAZIRI CHAMI USILALAMIKE. WANANCHI WANAWAOGOPA VIONGOZI WAO KAMA UKOMA KWA SABABU NDIYO MAZINGIRA VIONGOZI WA SERIKALI YALIYOJIJENGEA. ITATOSHA TU KUELEZA KWAMBA MBAO NI KWA AJILI YA SHULE NA NADHANI WATU WATAKUELEWA, ILI MRADI TU HUNA HISTORIA INAYOTIA SHAKA. HONGERA MWANDISHI ALIYETHUBUTU KUTOA TAARIFA HII!

    ReplyDelete
  2. Tutajuaje Bwana? Unasema ulipewa kibali ukawaachia wengine wavune. Tutajuaje wewe hauko nyuma yake? Vipi mbao kutoka Iringa kwenda kujenga shule Kilimanjaro? Unamndanganya nani? Hao uliowapa kibali chako walizipeleka wapi?

    ReplyDelete
  3. Jamani Tanzania ni zaid tuijuavyo. yaani watu wanatoa majibu rahisi kwa maswali magumu. huyu amefuatisha aliyosema Lukuvi sasa kila mtu atasema anataka kwa ajili ya shule jimboni mwake. Anasema aliwachia wengine huko si ndio kuuza vibali kwenyewe. Arudi akijipange aje na uongo mwingine unaokaribia ukweli.

    ReplyDelete