15 December 2010

Simba, Yanga 'dugu moja'

*Zapanga kushirikiana kimataifa

Na Elizabeth Mayemba

TIMU za Simba na Yanga zimepanga kushirikiana katika michuano ya kimataifa ili waweze kufanya vizuri na kuipeperusha vema bendera ya taifa katika michuano hiyo.Simba inawakilisha nchi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, baada ya
kuwa mabingwa wa Bara msimu uliopita, na Yanga wanashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), baada ya kushika nafasi ya pili.

Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu ya Simba, Clifford Ndimbo, alisema viongozi wa timu hizo, juzi walikutana kwa ajili ya kula chakula cha mchana pamoja, na kuzungumzia ushiriki wao katika michuano ya kimataifa.

"Tumeamua tushirikiane katika michuano ya kimataifa ili kila mmoja afanye vizuri, tutakuwa tukipeana mawazo na ushauri kwa kila timu itakapokuwa ikicheza," alisema Ndimbo.

Alisema wanawataka mashabiki wa timu hizo kuwa na ushirikiano wakati timu moja itakapokuwa ikicheza, ili kuwaunga mkono wachezaji, kusiwepo na tabia ya kuwashangilia wageni.Ndimbo alisema katika mechi za Ligi Kuu, U-Simba na U-Yanga utabaki pale pale, kutokana na upinzani mkali uliopo kwa timu hizo.

Wakati huo huo, klabu hizo mbili zimewapongeza viongozi wapya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Katibu Mkuu,  Angetile Oseah na Msemaji wa shirikisho hilo, Boniface Wambura.

"Tuna imani viongozi hawa watatoa ushirikiano kwenye klabu zetu, hasa katika suala la mapato ambalo limekuwa likilalamikiwa sana," alisema.

No comments:

Post a Comment