Na Mwali Ibrahim
KAMPUNI ya Benchmark Production, jana imewakabidhi zawadi washindi sita wa kinyang'anyiro cha kusaka vipaji vya muziki 'Bongo Star Search', kilichomalizika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa
kampuni hiyo, Ritha poulsen, alisema mashindano hayo yalifanyika kwa haki na mshindi alipatikana kihalali, na kwamba, mbali ya fedha taslim, washindi wote waliofikia hatua ya kumi bora watapata nafasi ya kurikodiwa video ya nyimbo zao watakazozitunga katika studio za MJ Records.
Alisema kampuni yake inajipanga kuhakikisha inaweka mipango mizuri ya kuwaendeleza washindi hao katika muziki.
"Nashukuru mashindano yalikwenda vizuri, ingawa baadhi ya watu wanadai kulikuwa na upendeleo katika kumchagua mshindi, lakini wanatakiwa kutambua mshindi huyo alipatikana kihalali kwani kura za majaji na mashabiki zilikwenda sawa" alisema Ritha.
Mshindi wa kwanza Mariam Mohamed, alikabidhiwa hundi yenye thamani ya sh. milioni 30, hospitali ya AAR kumgharamia yeye na familia yake matibabu yenye thamani ya dola 15,000 ndani au nje ya nchi kwa muda wa miaka miwili.
Pia, duka la Mariedo Botique, lilijitolea kumvalisha nguo zenye thamani ya sh. milioni moja.
Mshindi wa pili, James Martin, alipata sh. milioni 10, akifuatiwa na mshindi wa tatu, Joseph Payne, aliyeondoka na cheki ya sh. milioni 5 na sh. milioni moja ilikwenda kwa Christabella Kombo.
Waziri Salum na Ruth Oscar, kila mmoja alipata sh. milioni moja, Salum ni kwa ajili ya kuwa mshindi wa tano na Ruth ni kuwa na nidhamu katika kipindi chote cha miezi miwili ya mashindano hayo.
Alisema, mchakato wa kurekodi video ya nyimbo za washiriki utaanza baada ya sikukuu za Krismas na Mwaka mpya.
No comments:
Post a Comment