22 December 2010

Tanzania, Kenya zatoka sare

KIGALI, Rwanda

TIMU ya taifa ya vijana wenye miaka chini ya 17 ya Tanzania (Serengeti Boys), juzi ilitawala mchezo wao dhidi ya Kenya, lakini ilibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2, katika Uwanja wa Nyamirambo, Kigali, Rwanda. Serengeti Boys ilipoteza
mechi ya kwanza dhidi ya Rwanda, baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, Jumamosi.

Hata hivyo katika mchezo dhidi ya Kenya, timu hiyo ilianza kwa kuwapa hofu mashabiki wake, baada ya kuruhusu penalti dakika ya kwanza iliyofungwa na Joseph Wanyonyi.

Dakika tisa baadaye, Serengeti Boys iliingia katika wakati mgumu baada ya Kondo Hassan kuoneshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje na mwamuzi kutoka Rwanda,  Issa Kagabo.

Lakini wakati mechi ikionekana kama Serengeti Boys watapoteza, walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 19, kwa shuti lililompita kipa wa Kenya, Fred Odhiambo.

Dakika ya 29, Serengeti Boys walipata bao la kuongoza lililofungwa kwa kichwa na Habib Rashid.Kenya walijibu mashambulizi na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 55, lililofungwa na Martin Lemayian aliyeunganisha mpira wa krosi uliopigwa na Andrew Murunga.

Wakenya dakika tano za mwisho, walicheza pungufu, baada ya  Robinson Mwangi kutolewa nje kwa kumchezea vibaya mmoja wa wachezaji wa Serengeti Boys."Ilikuwa mechi nzuri na michuano mikubwa, lakini tulipata taarifa muda mfupi na kushindwa kujiandaa vizuri," alisema Jamhuri Kihwelu, Kocha wa Serengeti Boys.

Kwa upande wa Kenya Bob Oyugi,  alikuwa na furaha na matokeo hayo na kusema itakuwa timu tofauti, wakati tutakapovaana na Rwanda kesho.

Michuano hiyo maalumu ya timu tatu imeandaliwa na Wizara ya Vijana na Michezo ya Rwanda kuipa mazoezi timu ya taifa ya Rwanda itakayocheza fainali za Afrika kwa vijana wenye umri wa miaka chini ya 17, mwezi ujao.

No comments:

Post a Comment