08 December 2010

Wakana mashtaka ya kutakatisha fedha

Na Rabia Bakari

ALIYKUWA mhasibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw.Justice Katiti na wenzake watatu wanaokabiliwa na tuhuma za kutakatisha fedha haramu, zaidi ya sh. bilioni 3.8 wamekubali maelezo yao binafsi na kukana
mashtaka 11 yanayowakabili.Washtakiwa hao walikana makosa yanayowakabili wakati wakisomewa maelezo ya awali jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa Mwandamizi wa Serikali, Bw. Fedrick Manyanda mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Ritha Tarimo.

Bw. Katiti alikubali kuwa yeye ni mkazi wa Dar es Salaam, ambaye aliajiriwa TRA mwaka 2008 na kwamba anafanya kazi kama Mhasibu Msaidizi wa kitengo cha kodi kubwa (Large Tax Payers Department).

Mshtakiwa wa pili Bw. Samweli Renju alikubali maelezo yaliyosema kuwa yeye ni mkazi wa Dar es Salaam, ambaye mwaka 2008 aliajiriwa na benki ya NBC kama Meneja wa Tawi la Victoria jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa mshtakiwa wa tatu Bw. Haggay Mwatonoka alikubali kuwa yeye ni mkazi wa Dar es Salaam, mwaka 2008 na aliajiriwa na benki ya NBC tawi la Victoria kama mhasibu wa tawi hilo, huku mshtakiwa wa nne, Bw. Hope Lulandala naye alikubali kuwa yeye ni mkazi wa Dar es Salaam, na mnamo mwaka 2008 aliajiriwa na benki ya NBC tawi la Victoria kama mshauri wa mauzo.

Baada ya washtakiwa hao kukiri maelezo binafsi walikana mashtaka yafuatayo kwa ujumla wake.

Katika mashtaka ya msingi, washtakiwa wote kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Mei na Novemba mwaka 2008 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kuiba fedha TRA, na kuzihamishia kwenye akaunti za makampuni mbalimbali na ya watu binafsi huku wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa la jinai.

Pia wanadaiwa kuwa mnamo Juni 6, 2008 wakiwa ni waajiriwa katika ofisi za umma, waliiba sh 960,148,290.15, Septemba 18,2008 waliiba fedha nyingine sh 1,426,450,684.05 na  Novemba 20, mwaka huo waliiba tena sh 1,415,418,801.37 mali ya TRA.

Wanadaiwa kuwa kati ya Mei na Novemba, 2008 walikula njama kwa kushirikiana na watu wengine wasiojulikana kutakatisha fedha haramu kinyume cha sheria.

Wanaendelea kudaiwa kuwa kati ya  Mei na Juni, 2008 walihamisha Sh. 960,148,290.15 kutoka kwenye akaunti namba 07410300033 ya Benki ya NBC kwenda akaunti namba 074103000112 ya NBC ya Kampuni ya Express Booking Enterprises na akaunti namba 074103000276 ya NBC ya Kampuni ya TAC Traders Limited na akaunti namba 074103000100 ya NBC ya Daima Pharmaceuticals na watu wengine.

Kati ya Septemba na Oktoba, washtakiwa hao wanadaiwa kuhamisha  kutoka kwenye akaunti namba 07410300033 ya NBC ah. 1,426,450,684.05 kwenda kwenye akaunti 074103000112 ya NBC ya Kampuni ya Express Booking Enterprises na kwenye akaunti namba 074103000276 ya NBC ya Kampuni ya TAC Traders Limited na kwenye akaunti namba 074103000100 ya NBC ya Daima Pharmaceuticals na watu wengine.

Katika shtaka lingine washtakiwa hao, pia wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba na Novemba, walihamisha fedha kutoka kwenye akaunti namba 07410300033 ya NBC sh  1,415,418,801.37 kwenda akaunti 07410300033 ya NBC ya Kampuni ya Express Booking Enterprises, kwenye akaunti namba 074103000276 ya NBC ya TAC Traders Limited na akaunti namba 07410300033 ya NBC ya Kampuni ya Daima Pharmaceutical na watu wengine.

Baada aya hatua hiyo, Wakili Manyanda aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo, ambapo pia upande wa mashtaka utapata nafasi ya kutaja idadi ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika kuendesha kesi hiyo.

Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 21, mwaka huu ambapo itatajwa.

1 comment:

  1. Hatutashangazwa kabisa kusikia na kesi kubwa kama hii kutohukumiwa kihalali. Kwa kweli Tanzania haiaminiki tena. Hajulikani yupi wa kuaminika.... NOT ANYMORE!

    Watanzania wakawaida wanapata tabu bure kutia kura.... Maana hao wanaowachagua ndio walaji wakubwa na wao ndio watalifunika jambo kama hili. Wacha tuone basi...

    WEWE vipi ifike kiasi cha pesa kikubwa kama hivi kuibiwa kama wakubwa hawamoooo? Kazi kwa Jaji, na yeye hatujui, Mungu anajua!

    ReplyDelete