08 December 2010

Japan yatoa msaada wa mil 764/-

Na Agnes Mwaijega

SERIKALI ya Japan imetoa msaada wa sh milioni 764 kwa ajili ya miradi ya maendeleo vijijini katika mikoa sita nchini.Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha Afya Mkuranga, mabweni ya wasichana Shule ya Sekondari
Mwalimu Nyerere Wilaya ya Kahama, Shinyanga; Msakwalo Wilaya ya Kondoa Dodoma; Matogoro Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma; zahanati katika Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na kupanua kituo cha afya katika Wilaya ya Longido mkoa wa Arusha.

Akizungumza Dar es Saalam jana wakati wa kusaini mkataba wa makubaliano na wawakilishi kutoka katika mikoa hiyo, Balozi wa Japan nchini, Bw. Hiroshi Nakagawa alisema kutokana na sheria za ubalozi, wao wanatakiwa kukamilisha ujenzi huo baada ya mwaka mmoja tangu kutolewa kwa msaada huo.

Alisema wanaiomba serikali ya Tanzania kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa miradi yote unakamilika kwa wakati.Bw. Nakagawa alisema chini ya mradi wao unaotoa msaada wa kifedha kwa nchi zinazoendelea (GGHSP), watahakikisha wanafuatilia utekelezaji mpaka ukamilike.

"Tutafuatilia utekelezaji mpaka tuhakikishe kazi yote imekamilika na tutahitaji ripoti kwa kila hatua itayofikiwa," alisema balozi huyo.  Aliongeza kuwa kutatua matatizo ya kimaendeleo vijijini ni muhimu kwa sababu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.Nao waalimu wakuu kutoka shule za sekondari Matogoro, Mwalimu Nyerere na Msakwalo walisema ujenzi wa mabweni utaongeza kiwango cha wasichana kufaulu.

Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige alisema atahakikisha anasimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi hiyo mpaka ikamilike.

No comments:

Post a Comment