08 December 2010

Taasisi ya India kuwanoa madaktari nchini

Na Reuben Kagaruki

TAASISI ya HCG Group ya nchini India imeahidi kutoa mafunzo kwa madaktari na wauguzi wa Tanzania kuhusu tiba ya saratani na imeonesha nia ya kushirikiana na Wizara ya Afya nchini kwa ajili ya kuanzisha vituo vya kutibu saratani mikoa yote
nchini.

Hayo yalisemwa Mwenyekiti wa Regency Medical Center , Dkt. Rajni Kanabar, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana.

Alikuwa akizungumzia makubaliano ambayo Hospitali ya Regency imeingia na taaasisi ya Health Care Global Enteprises, ambayo ni maarufu kwa kutibu saratani duniani.

Taasisi hiyo ina mtandao wa vituo 22 sehemu mbalimbali duniani, ikiwemo India na Asia ya Kusini na inatarajia kuongeza matawi yake nchi za Tanzania, Angola, Uganda na Nigeria kwa kuweka vituo vya kisasa vya kutibu saratani.

Dkt. Kanabar alisema watashirikiana na serikali ya Zanzibar ili kubaini mapema saratani ili iweze kutibika vizuri totafuti na sasa ambapo watu wengi wanachelewa kwenda hospitali.

"Sisi hapa Regency tunaamini mpango huu wa ushirikiano na HCG Group wa kushirikiana na sekta ya umma na binafsi utaongeza jitihada za serikali katika utoaji wa huduma kwa watu wenye saratani," alisema.

"Tunaishukuru Wizara ya Afya kwa kuwezesha ushirikiano huu ambao utakuwa fursa nyingine kubwa kwa hospitali ya Regency katika kutoa huduma zake," alisema Dkt. Kanabar.

Naye mtaalamu wa maradhi ya saratani kutoka HCG Group ya mji wa Bangarole India, Sridhar Papaiah, aliendesha kambi ya siku mbili katika hospitali ya Regency kuchunguza watu wenye saratani na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Alisema tangu juzi ameshawachunguza watu 50 na kati ya hao amebaini kuwa watano wana matatizo ya saratani.

No comments:

Post a Comment