29 December 2010

Vuai akemea kampuni binafsi kuzima moto kwa milioni 5/-

Na Peter Mwenda

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Bw. Shamsa Vuai Nahodha ameshangazwa na utaratibu wa Kampuni ya Night Support kutoza sh. milioni 5 kwa huduma ya kuzima moto nyumba yenye thamani ya sh. milioni 10 .Akizungmza katika ziara yake
ya kukagua utendaji kazi wa kampuni binafsi za kuzima moto Dar es Salaam jana, Bw. Nahodha alisema janga la moto si anasa inakuwaje kampuni hiyo imtoze kiasi chote hicho mwananchi ambaye hajajua kama nyumba na mali zake zitasalimika.

"Hampo katika kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania mpo kibiashara, Serikali haiwataki mtoe huduma ya kuzima moto bure, lakini mnapochaji sh. milioni 5 hiyo ni biashara kubwa," alisema Bw. Nahodha.

Bw. Nahodha aliyetembelea Kampuni ya Ultimate Security, Security Group na Night Support kuona utendaji wao na msaada wa kampuni hizo wakati wa matukio ya moto kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam, 'aligeuka mbogo' baada ya maelezo ya wamiliki wa kampuni hizo kurushia mzigo Kikosi cha Zimamoto.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Knight Support Tanzania Ltd, Bw. David Sutton 'aligeuka mbogo' wakati mazungumzo yakiendelea baada ya Kamishna Mkuu wa Zimamoto, Bw. Matwani Mohamed kueleza kuwa kampuni hiyo hugoma kwenda kuzima moto mpaka kwanza walipwe sh. milioni 5.

Kauli hiyo ilimfanya Bw. Sutton kuja juu na kuamka kwenye meza aliyokuwa amekaa na Waziri Nahodha huku akitishia kuondoka katika meza hiyo lakini alijirudi na kukaa ambako aliomba radhi na mazungumzo kuendelea.

Kitendo hicho kilimkasirisha Waziri Nahodha na kumwambia mwekezaji huyo ajue yupo kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa Tanzania mbali ya utetezi wake kuwa amewahi kuzima moto maeneo mengi bila kudai fedha.

Waziri Nahodha alionesha waziwazi kuwa kitendo hicho alichofanyiwa hakikupendeza hivyo aligoma kula chakula kilichoandaliwa kwa ajili yake na msafara wake na kusisitiza kuwa watendaji wa Bodi ya Zimamoto ndiyo wenye kasoro katika utendaji wao.

"Je, unajua sera na sheria za leseni yako? Zinakutaka wewe ufanye nini? Bw. Sutton alishindwa kujibu na swali hilo kuelekezwa kwa Kamishna Bw. Matwani na kumtaka aeleze mkataba kati ya kampuni binafsi na Serikali kuhusu wanachotakiwa kuchangia wakati wa kuzima moto ambaye pia hakutoa jibu sahihi.

Kutokana na kutopatikana jibu sahihi, Waziri Nahodha aliagiza Kikosi cha Zimamoto na Bodi yake kipindi cha wiki moja kutengeneza sera ambazo zinapaswa kufuatwa na kampuni binafsi.Mkurugenzi huyo wa Knight Bw. Sutton alisema endapo akiingia mkataba wa kuzima moto katika Jiji la Dar es Salaam atahitaji kulipwa sh. bilioni 6.5 kwa mwaka.

"Leseni yako unasema unalipia sh. 500,000 inakuweje utoe huduma kwa dola milioni  5 (sawa na Sh. bilioni 6.5 kwa mwaka?" alihoji Bw. Nahodha.
Kabla ya Knight Support, Waziri Nahodha alitembelea kampuni ya Ultimate Security na Security Group ambako waliomba Serikali ijenge matangi ya kuhifadhia maji kwa ajili ya matumizi ya kuzima moto pindi linapotokea janga hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Ultimate Security, Bw. Zainul Dossa alisema kampuni hiyo inakabiliwa na changamoto za ufinyu wa barabara wakati wa kwenda kuzima moto na vipuri vinavyoagizwa nje kwa ajili ya injini za kunyunyiza maji ni ghali sana.

2 comments:

  1. Mimi naona hizi kampuni zinapaswa kuchunguzwa au sera nzima ya zimamoto iangaliwe, tusiamue kujenga majumba makubwa wakati hatujui iwapo utatokea moto tutaushughulikia vipi. Hizi kampuni zote hazina lengo nzuri maana wanapofika kwenye ajali ya moto hawakubali kuanza kuzima moto mpaka usaini kua umekubali kulipa mamilioni ya pesa ili kupata huduma yao. Unafikia kuambiwa usaini utalipa hata shs milioni 50 kama jengo lako kubwa wakati haujui watafanikiwa kuuzima moro ama watashindwa

    ReplyDelete
  2. Vuai, kazi za uokoaji na zimamoto si shuguli za lelemama. Huwezi ku price roho ya mwanadam ingawa unaweza kwa nyumba na mali nyengine.

    Isitoshe, wacha Shs milioni 5, hata ingekuwa 25 si chochote kwani basic idea ni kuokoa maisha.Wenzetu wanatumia zaidi ya Shs Milioni 5 kuokoa paka au kiji-mbwa kilichokwama kwenye mtaro au mti.

    Ikiwa unahisi hii ni kazi ya profit & loss, na unaona fedha zinakuuma, wape vifaa na wafundishe zimamoto wa serikali na hapo tutajivunia uongozi wako!

    ReplyDelete