16 December 2010

TP Mazembe yaweka rekodi, yatinga fainali Kombe la Dunia

ABU DHAB, Falme za Kiarabu

MABINGWA  wa Afrika,  TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC),  wamefuzu fainali ya Kombe la Klabu Bingwa Duniani baada ya kuwafunga mabingwa wa Amerika ya kusini,  Internacional kutoka Brazili mabao 2-0 mjini
Abu Dhabi.

TP Mazembe inakuwa klabu ya kwanza barani Afrika kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Dunia, inasubiri kucheza fainali dhidi ya mshindi kati ya mabingwa wa Ulaya, Inter Milan ya Italia na mabingwa wa Asia, Seongnam IIhwa kutoka Korea Kusini, ambazo zilitarajiwa kuchuana jana katika nusu fainali ya pili ambapo fainali hiyo itafanyika Jumamosi ijayo.

Bao la kwanza la TP Mazembe,  lilifungwa  dakika ya 53 na Mulota Kabangu, naye Dioko Kaluyituka akafunga la pili dakika ya 85.

Internacional walipata nafasi nyingi katika kipindi cha kwanza, lakini ngome kali ya ulinzi ya TP Mazembe ambayo ilizuia  mashambulizi yote, huku pia mlinda mlango Muteba Kidiaba, akiokoa mikwaju mingi.

Mbali na kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kutinga hatua hiyo, vilevile TP Mazembe inakuwa timu ya kwanza kutoka nje ya Ulaya na Amerika Kusini, kufika mbali katika mashindano hayo.

"Tupo hapa kuiwakilisha Afrika na Waafrika wote, tunapaswa kujivunia kazi yetu," alisema kocha wa TP  Mazembe, Msenegal, Lamine N'Diaye.
"Ni siku ya furaha kwetu na vilevile ni siku ya kujidai tumefanikiwa na tumeomesha kuwa, wachezaji wetu wapo katika kiwango cha hali ya juu," aliongeza.Awali, ilionekana  kama itakuwa miujiza kwa timu hiyo kusonga mbele kutokana na kuanza vibaya kipindi cha kwanza, huku kipa Kidiaba akionekana kusimama kidete na kujiamini kuwapunguza makali Internacional.

Pamoja na uoga, mbali na jitihada binafsi za mchezaji, Kaluyituka  timu hiyo kutoka DRC, kipindi cha kwanza ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi,  lakini mchezo ulipokuwa ukiendelea,  TP Mazembe walianza kujiamini na kufanya mashambulizi pamoja na kujilinda.Kuongeza kwa kujiamini kulionekana wakati mchezaji  Kabangu, alipopokea pande safi akiwa nje ya eneo la hatari na kutuliza vyema mpira huo, kisha kuachia mkwaju pembeni mwa goli na kumuacha kipa wa Internacional, Renan, akiwa ameduwaa.

Mabadiliko  ya kuwatoa wachezaji wawili, Tinga na Alecsandro, na kuwaingiza wachezaji chipukizi Giuliano na Damiao, yalionekana kuwapa uhai Internacional, lakini hata hivyo, hawakuweza kupata nafasi ya kusawazisha.

1 comment:

  1. Nice,Tabora
    Hongera TP Mazembe,Timu zetu Simba na Yanga zijifunze,Mpira ni Ushindi na wala sio makelele tuu.

    ReplyDelete