16 December 2010

Hall atangazwa rasmi Azam FC

Na Addolph Bruno

UONGOZI wa klabu ya Azam FC jana,  ulimtambulisha rasmi Kocha Stewart Hall,  kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.Kocha huyo amechukuliwa kuinoa Azam FC, baada ya klabu hiyo kusitisha makataba na aliyekuwa
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Itamar Amourin, mwezi uliopita na kulazimika kumsaka kocha mwingine.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Said Mohammed, alisema wamemnyakua kocha huyo baada ya kuona ana vigezo wanavyovitaka.

Alisema, awali walijitokeza makocha 25 kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi, lakini Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kazi hiyo chini ya Mwenyekiti wake,  Nassoro Idrissa, ilipendekeza majina matatu tu.

"Baada ya mchujo huo, lilikuwepo jina la Charles Boniface wa Tanzania, Steven Cash wa Nigeria na Michael David wa Ujerumani, lakini tukaona kocha anayefaa zaidi ni Stewart," alisema Mohammed.

Kwa upande wake Stewart, alisema amefurahi kujiunga na Azam FC, na kusisitiza kuwa, ni kutokana na viongozi na wachezaji kuwa na uelewa.
Kuhusu mkataba wake na timu ya Taifa ya Zanzibar 'Zanzabar Heroes', aliyokuwa akiifundisha, Stewart alisema ataendelea kuisaidia katika nyanja mbalimbali atakapopata nafasi ikijiandaa na michuano ya kimataifa itakayokuwa ikiwakabili.

Katika hatua nyingine, kocha huyo alianza kazi ya kuifundisha klabu hiyo jana katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mazoezi ya timu yake, alisema hawezi kugundua mapungufu katika kikosi hicho na safu ambayo anatakiwa kuifanyia kazi mpaka kesho, wachezaji wa kimataifa watakapounga na wenzao.

No comments:

Post a Comment