15 December 2010

Tibaijuka kumekucha!

*Arudisha maeneo Palm Beach na Ocean Road Dar
*Aamuru kuta zivunjwe na zitengenezwe bustani
*Eneo la Joseph Mungai,Msasani nalo lachukuliwa
*Apiga marufuku maeneo kutumika kinyume na ramani
*Atumia usafiri wa 'daladala' kutembelea maeneo


Na Grace Michael

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka ameagiza uongozi wa Manispaa ya Ilala kuvunja kuta
zilizojengwa katika maeneo ya wazi yaliyopo Ocean Road na Palm Beach jijini Dar es Salaam huku akiamuru maeneo kadhaa kurudishwa katika matumizi yake kama inavyoonekana kwenye ramani.

Mbali na agizo hilo, amesisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayeruhusiwa kutumia kiwanja chochote nje ya matumizi yanayooneshwa kwenye ramani kwa kuwa ndio inayoamua eneo litumike kwa matumizi gani.

Prof. Tibaijuka alitoa maagizo hayo jana Dar es Salaam alipotembelea maeneo mbalimbali ya wazi ya jiji katika ziara aliyoambatana na wataalam mbalimbali wa Wizara hiyo, baadhi ya wabunge, wakurugenzi wa manispaa pamoja na wakuu wa wilaya.

Katika ziara hiyo, tofauti na utaratibu unaotumiwa na watendaji wengi wa ngazi kama yake kuwa na misafara ya magari mengi ya kifahari ya watendaji( mashangingi), Waziri Tibaijuka na ujumbe wake, walipanda mabasi madogo mawili 'daladala' ya kukodi kutoka kampuni ya Aurora.

Akiwa katika kiwanja namba 59 kilichopo Ocean Road, aliamuru kuvunjwa kwa ukuta uliozungushiwa eneo hilo baada ya kupata maelezo na ramani kuonesha eneo hilo kuwa la wazi.

“Nadhani hapa hakuna mjadala kinachotakiwa ni kuvunjwa kwa huu ukuta kwani haya maeneo ni ya kila mwananchi kuyatumia, ni maeneo ya wazi ambayo yanatakiwa kujengwa bustani ili kila mtu aje na kufuarahia maeneo ya nchi yake...na kama kuna kesi mahakamani ni rahisi kwa kuwa Mahakama haina mamlaka ya kupanga mipango miji,” alisema Prof. Tibaijuka.

Historia ya kiwanja hicho ilielezwa kuwa kilimilikishwa kwa Jumuiya Shree Hindu Mandal mwaka 1952 kwa matumizi ya kuchomea maiti na mwaka 1967 shughuli za kuchoma maiti zilihamishwa lakini hati haikuwahi kufutwa.

Akieleza hayo Mkurugenzi wa Mipango Miji, Bw. Albina Burra alisema kuwa katika hali ya udanganyifu wamiliki hao wa awali waliibuka na kudai mabadiliko ya matumizi ya kiwanja hicho na baadaye Rais alikubali kufutwa kwa hati hiyo na kiwanja hicho kuachwa kama eneo la wazi.

Katika eneo la Palm Beach ambalo historia yake ilionesha kuwa na mgogoro ambao ulifika na kuamriwa na mahakama, napo aliamuru pavunjwe kwa kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa alishatengua umiliki wa eneo hilo kutoka kwa wamiliki wawili waliojulikana kama Shantaben Patel na G. Patel.

Kiwanja hicho namba 1006, kilibatilishwa rasmi mwaka 2002 na kufutwa umiliki wa hati ya kiwanja hicho na kuwa katika matumizi ya umma.

Hata hivyo baada ya ubatilisho huo, wamiliki hao wa awali walifungua kesi mahakamani wakishirikiana na Bw. Taher Muccadam wakiomba kutenguliwa kwa ubatilisho huo.

Akizungumzia mchakato huo, Prof. Tibaijuka alisema kuwa hakuna aliye juu ya Rais na kama Rais Mkapa alibatilisha umiliki huo basi hakuna namna na kinachotakiwa ni kuvunjwa kwa ukuta uliopo na nyumba iliyojengwa ndani yake lakini pia akatoa amri kwa Manispaa kupanda miti iliyokatwa na anayejidai mmiliki wa eneo hilo.

Sehemu nyingine aliyotembelea ni kiwanja namna 1072 kilichopo Upanga ambapo eneo hilo lilibuniwa bila kufuata utaratibu halijawahi kupimwa kwa kuwa ni kiwanja ambacho kipo katika eneo la mikoko na pia kiwanja hicho hakina sifa ya kuwa kiwanja kwa kuwa hakina barabara ya moja kwa moja.

Katika eneo la Oysterbay Beach, Prof. Tibaijuka alitoa maagizo kwa viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha wanakutana na wadau wote ili kuangalia ni namna gani wanaweza kulitumia eneo hilo na wananchi nao wakanufaika na pasiwe na manung’uniko yoyote.

Eneo jingine ambalo ilionekana umiliki wake ni wa utata ni la Msasani Village kiwanja namba 586 na 587 Kitalu 'F', eneo hilo awali lilimilikishwa kwa Shia Ithnasheri na baadae kuhamishiwa miliki yake kwa Bw. Joseph Mungai ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Ilielezwa kuwa taratibu za kubadilisha matumizi kutoka eneo la wazi kuwa makazi hazikufuatwa hatua iliyofanya kibali cha ujenzi kutotolewa na Manispaa.

Kutokana na maelezo hayo, Prof. Tibaijuka alisema kuwa katika hilo ni lazima watendaji wakiri kuwa walizembea katika kulishughulikia na hati ya hapo ni batili na eneo hilo linatakiwa kubaki katika matumizi yanayoonekana katika ramani ambayo ni pamoja na ujenzi wa Taasisi.

Mbali na maeneo hayo, pia alitembelea eneo ambalo makazi yake hayako kwenye mpangilio unaotakiwa katika eneo la Msasani Bonde la Mpunga ambapo alisema kuwa Serikali ni lazima iangalie namna ya kuwapa nyumba wakazi wa maeneo hayo ili eneo hilo liweze kupimwa na kuwekwa katika mpangilio unaofaa.

“Hapa ni lazima tuangalie wananchi tunawawezeshaje, kwani wapo ambao wana biashara zao hapa hivyo huwezi ukawaweka mbali au ukasema unawapa viwanja huko mbali...kinachotakiwa ni kuwapa nyumba na eneo kupimwa na hapa nataka uwe mfano,” alisema Prof. Tibaijuka.

Eneo jingine ambalo alitoa maelezo kama hayo ni la Bonde la Msimbazi ambapo alisema kuwa ni lazima wadau wote washirikishwe ili kuona wananchi wanachokihitaji kama ni nyumba au kiwanja na akatoa mwito kwa Shirika la Nyumba na mashirika mengine kujenga nyumba ili ziweze kusaidia.

Akizungumza baada ya kutembelea maeneo hayo, alisema kuwa kazi haziwezi kwenda bila kufika katika maeneo husika na kuona kama mipango iliyopo ofisini inalingana na iliyoko katika maeneo husika.

“Ni lazima utoke na uone kilichopo nje...hatuwezi kufanya kazi kama mangimeza kwa kukaa ofisini tu lakini katika mambo ya maeneo ya wazi hatuna muda wa kuleana tena...kitakachoamua ni kilichopo kwenye ramani yetu na si vingine hivyo hata wananchi wasitapeliwe ovyo ovyo waombe ramani na kuona kilichopo,” alisema.

Alisema kuwa ziara hiyo imejikita katika kushughulikia ripoti ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Willium Lukuvi na muda wa mwisho waliopewa wenye maeneo hayo ni mwisho wa mwaka huu na endapo watakaidi, wasitarajie kuambulia hata tofali.

Kwa upande wa Mbunge wa Ubungo Bw. John Mnyika ambaye naye alikuwa kwenye ziara hiyo, alisema kuwa mchakato huo pia unatakiwa ufanyike katika maeneo ya Ubungo kwa kuwa yapo maeneo ya wazi yanayotumika kinyume na matumizi na akaomba ripoti ya Bw. Lukuvi kuwekwa wazi ili ufuatiliaji uwe rahisi.“Mbali na haya lakini pia tungewaomba wenzetu wa Wizara kutengeneza mipango miji ya muda mrefu ili kuondokana na usumbufu,” alisema Bw. Mnyika.

14 comments:

  1. kama kazi hii itatekelezwa kadiri ya maneno haya ya prof Tibaijuka, basi tanzania itakwenda mbali kwa kupitia yeye kua mfano wa viongozi wengine! Mungu akupe nguvu ya utekerezaji prof Tibaijuka

    ReplyDelete
  2. Safi sanaa mama mkwe,hatuichukii CCM ila tunataka watu wafanye kazi kwa manufaa ya wananchi wa kawaida,angalia isiwe nguvu ya soda mama,kaza buti mheshimiwa ni mwanzo mzuri.

    ReplyDelete
  3. Kwa kasi hii ya maongezi tumeiona na tunashukuru sana maana duh! we acha tu mama Tibaijuka lakini Vitendo vitakuwepo? sisi tunakusubili tu kama havitakuwepo basi wakati ukifika na sisi tuta amua

    ReplyDelete
  4. Bavoo Mamaa Tibaijuka,hongera sana mama,wewe ndio aina ya viongozi tunaowataka maana wahanga wa kubomolewa nyumba siku zote walikuwa walalahoi tu,umenikosha kwa kusema lazima muangalie jinsi ya kusaidia watakaoathirika hapo bondeni na kujadiliana nao. kingine ni hao jamaa wa National Housing Corp,inabidi uwavalie njuga,hili ni shirika la umma lilianzishwa kwa makusudi ili lisaidie wanyonge,mfano ni nyumba za Magomeni na Kinondoni,lakini hawa jamaa sasa wamejikita na matajiri tu na mfano hai ni huu,serikali ilitoa idhini ya shirika hili kuingia ubia na wenye majumba mjini ili kujenga maghorofa ili kukidhi hali ya makazi,jamaa hao ikawa kama wamefunguliwa neema ya kujitajirisha,hapa hakuna masikini anyepata na hawa jamaa ila ni Waasia matajiri ndio wanaoingia ubia na shirika hili la umma na kujengewa maghorofa makubwa,hivi kweli tunakwenda wapi,aliyenacho anaongezewa na asiyenacho anakandamizwa,huyu mlalahoi hata akitaka kurepea nyumba yake anakatazwa ati mpaka awe na plan ya ghorofa na ajenge ghorofa
    na matajiri wamezidhibiti halmashauri za miji ili kuwabana masikini wenye majumba mabovu ili wazinunue wao,hasa mji wa Arusha umekithiri kwa hilo,njoo huku uturekebeshia hii halmashauri. AHSANTE SANA MAMA KWA KAZI NZURI MATAJIRI WATAKUPIGA VITA LAKINI SISI TUPO PAMOJA NA WEWE. BADILISHA MWELEKEO WA SHIRIKA LA NYUMBA ILI LIWE LA MASIKINI

    ReplyDelete
  5. AMA KWELI TUMEPATA RAIS MWANAMAMA MWAKA 2015. ILA TUONE MATENDO YATIMIE. SASA HATA MUNGAI WAZIRI MZIMA ANAKUWA MVUNJA SHERIA?? HII NDIYO ILNAYOTUAANGUSHA CCM!HONGERA MAMA NA MUNGU AKULINDE. TUNAMWOMBA RAIS KIKWETE AKUPE MSAADA NA ASIWE KIKWAZO.

    ReplyDelete
  6. Nampongeza sana Prof. Mama Tiba, ila wasiwasi wangu ni kama kweli watendaji wake watatekeleza hayo? Miaka mingi tumeshuhudia viongozi wengi wanaanza kama vile lakini baadaye tunapewa maelezo kuwa Waziri alichemsha.

    ReplyDelete
  7. Povu la mkojo. Jogoo wa shamba kamwe hawezi kuwika mjini na akifanya hivyo huwa uchuro.

    Tusubiri tuone. Nguvu za akina magufuli na baadae zikapotea na kuishia kuchoma nyavu za wavuvi masikini tu

    ReplyDelete
  8. pETRO eUSEBIUS mSELEWADecember 15, 2010 at 3:52 PM

    Mwanzo mzuri,katikati....,mwisho....

    ReplyDelete
  9. Unawaona mashetani hao wanaotoa mifano ya povu la mkojo,nchi hii ina mafisadi wengi tu ambao wananyooshea vidole wenzao,tayari wameishakuwa na hofu na wanaanza kumkatisha tamaa,hawa ni madalali wa hao waporaji ardhi sasa wanaona kitumbua kimeingia mchanga,wanaanza mawazo ya kebehi. ziko wapi NGO/wanaharakati/wailiokuwa mstari wa mbele wakati wa uchaguzi mkuu kusema kila wanaloliona na kukosoa kila jambo,hili lenye neema kwa walalahoi wako kimyaaa,mama tuko pamoja na wewe na wewe unayesema povu la mkojo jitayarishe wewe kukojoa povu la damu. siku zote hao wanaonufaika na uozo wa viongozi hujaribu kukatisha tamaa. BRAVOO MAMAA PLAY YOUR PART AND WE PLAY OUR PART IT CAN BE DONE

    ReplyDelete
  10. Sasa tuna Wizara mbili zilizoshikwa na viongozi wachapa kazi. Na siyo Waheshimiwa Watawala. Dr. Magufuli ( Ujenzi ) na Prof.Tibaijuka. Hawa watakuwa mfano kwa wenzao wanaoshinda maofisini na kwenda kwenye mikutano badala ya kufanya kazi.

    ReplyDelete
  11. Tatizo ni kwamba watu wachini tusije kukaonewa kwa sababu watu wengi tu tunaishi kama skwata. Kufuatilia upimaji ni kazi ngumu na ya kutoa rushwa. Sasa sisi wengine tulikuwa na mashamba muda murefu na tukawa tunapigwa mizengwe kwa muda murefu. Tunaomba tu haki na ubinadamu uzingatiwe

    ReplyDelete
  12. Mama nakutahadhari usianze kwa kasi kazi ikakushinda, walijifanya wakali kina Magufuli kazi ikawashinda hakuna kitu tulichoweza kukiona alichofaya zaidi ya kusoma katika magazeti jinsi gani alivyo mchapa kazi.Tatizo halipo na wamiliki wa hivyo viwanja au hizo nyumba bali lipo hapo kwako wizarani ndiyo wanaoyatembeza hayo maeneo ya wazi na nyumba za serikali kutaka kuviuza na kuwaahidi kuwashanghulikia mpaka kuvipata kisheria sasa bora kwanza ungeanza kuitisha mafaili na kutizama ni jinsi gani hivyo viwanja vya wazi vikafikia hapo tulipofikia vikagaiwa kwa watu binafsi, ila naomba uwe mwangalifu hakuna anae aminika hapo wizarani inabidi uifanye hiyo kazi mwenyewe vingine utapewa taarifa zao uongo kama waliokutangulia na kazi ikakushinda. Hayo maeneo yote kama utayatafiti yamegaiwa kisheria kwa msaada wa hao wafanya kazi wasio waaminifu wizarani kwa hivyo kwanza mama safisha wizara yako kabla ya yote.

    ReplyDelete
  13. Mama Tibaijuka namfahamu vizuri! Anachokisema anamaanisha! Na mtaona makubwa mengi! Anastahili kupewa ushirikiano wetu wananchi na Serikali Kuu!

    Tutafika tu!

    Ardhi ya matajiri?! Nani kasema!!!

    ReplyDelete
  14. Mama mkwe najua wewe ni mwadilifu tena sana na najua nia yako thabiti inadhamiria kuondoa kero pamoja na kufanya wananchi wako waishi maisha bora katika makazi bora ila lazima utambue kwamba utapigwa vita sana na watumishi wako wa hapo wizarani pampja wakubwa wenzako na hata wakubwa wako. Ushauri wangu ni kwamba chunguza vizuri na uende taratibu katika kutatua kero mbalimbali za ardhi. Kwakuwa una nia njema na mwenyezimungu wakati wote huwalinda waja wake wenye kukusudia kufanya yaliyomema inshaallah mungu atakuwa pamoja nawe. Sisi wenye mapenzi mema na nchi yetu pia tuko pamoja na wewe, ila ujue mama mkwe vipingamizi ni vingi maana kuna matajiri wa pesa na wenye madaraka (vyeo)! Hatari kwelikweli mama mkwe.

    ReplyDelete