15 December 2010

Askari magereza ajimiminia risasi kichwani, afa

Na Daud Magesa, Mwanza

ASKARI mmoja wa Jeshi la Magereza katika Gereza Kuu la Butimba Jijini Mwanza, amekufa papo hapo baada ya kujimiminia risasi tatu kichwani kwa kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG). Akizungumza jana na waandishi wa
habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Bw. Simon Sirro, alisema askari huyo namba B 5004, Elias Bukarima mwenye Cheo cha WRD, alijiuwa kwa kujipiga risasi saa 7 mchana kwa kutumia bunduki hiyo yenye namba 061220 aliyokabidhiwa kwa ajili ya kazi.

Alieleza kuwa kabla ya kujipiga risasi, askari huyo alikuwa akiwasiliana kwa simu na mtu ambaye hakufahamika jina na kudai ni miongoni mwa wanaomfanya aishi maisha ya shida. Kamanda Sirro alisema bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na jitihada za kumtafuta mtu aliyekuwa akiwasiliana na marehemu kwa simu muda mfupi kabla ya kifo chake.

Hata hivyo alieleza pamoja na kumsaka mtu huyo, bado kuna ugumu wa kumpata kutokana na namba ya simu hiyo kutopatikana hewani pindi ilipopigwa tena.Aidha katika tukio lingine wilayani Ukerewe mtu mmoja anadaiwa kufa kwa kipigo katika ugomvi ambao chanzo chake hakikuweza kufahamika mara moja.

Kamanda sirro alimtaja aliyekufa kuwa ni Mafwele Machumu (27) mkazi wa kijiji cha Muriti, Tarafa ya Ilangala wilayani Ukerewe ambaye alikufa baada ya kupigwa mateke na ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake. Alisema marehemu alipigwa na  Paulin Mritu (39) saa 6:45 mchana katika
kijiji hicho baada ya kutokea ugomvi ambao chanzo chake hakijafahamika.Kamanda Sirro alisema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na  tukio hilo na anasubiri kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

2 comments:

  1. inawezekanaje mtu alie piga simu asijulikane hali watu wame register namba zao za simu? na inakuwaje maongezi yasi fahamike mara moja hali kampuni ya mtandao wa simu alokua akitumia unajulikana? recodings si zipo? tupunguze uzembe katika swala la ulinzi Tz

    ReplyDelete
  2. Uongozi wa serikali usitake tuamini kuwa zoezi la usajili wa namba za simu ulikuwa danganya toto. Huyo mtu apatikane na achukuliwe hatua akikutwa na hatia, kwani hapo ni maisha ya mtu yamepotea, tena Askari

    ReplyDelete