Na Zahoro Mlanzi
SIKU moja baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kutoa ratiba ya mashindano ya kimataifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limezitaka Klabu za Simba na Yanga zijiandae mapema ili zifike mbali katika
mashindano hayo.
Simba itaiwakilisha nchi katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Afrika, ambapo imepangwa kuanza na Elan Club de Mitsoudje ya Comoro kati ya Januari 28 na 29 na 30 na kurudiana kati ya Februari 11, 12 na 13 mwakani na endapo itafuzu hatua hiyo itaumana na mabingwa watetezi TP wa Kombe hilo, Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
Wakati Simba ikijiuliza kwa Wacomoro, wawakilishi wengine katika Kombe la Shirikisho, Yanga wataumana na Debit ya Ethiopia na ikipita hatua hiyo itavaana na Haras El Hadoud ya Misri.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo, Sunday Kayuni alisema anazitaka klabu hizo zifanye maandalizi mapema kwa kutumia Ligi Kuu ya Bara, kwani ratiba imetoka wakati muafaka.
"Unajua baada ya michezo hiyo ya awali endapo zitashinda, hakuna shaka mashabiki wengi macho na masikio yao yatakuwa kwao kutokana na timu zitakazokutana nazo huko mbele, hivyo ni wakati mzuri klabu hizo kufanya maandalizi ya nguvu ili angalau zifike mbali hata robo fainali," alisema Kayuni.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), limewapa beji za kimataifa waamuzi 14 wa Tanzania baada ya kufaulu mitihani yao waliyofanya Septemba, mwaka huu.
Kayuni aliwataja waamuzi hao kwa upande wa kati kuwa ni Oden Mbaga, Israel Nkongo, Waziri Sheha na Ibada Sibo na wasaidizi wao ni Josephat Bulali, Hamis Chang'walu, Rongional Kanyenye, Jesse Erasmo, Kombo Ally, Hamis Marwa na Samuel Mpenzi.
Kwa upande wa wanawake ni Judith Gamba ambaye ni mwamuzi wa kati na Mwanahija Makame na Saada Tibabimale waamuzi wasaidizi.
No comments:
Post a Comment