20 December 2010

Tanzania yapanda viwango vya netiboli duniani

Na Amina Athumani, Kibaha

TANZANIA imepanda viwango vya kimataifa vya mchezo wa Nnetiboli vinavyotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Netiboli (IFNA), kutoka nafasi ya 24 hadi nafasi ya 20.Pia, imepanda kutoka nafasi ya nne hadi nafasi ya tatu kwa ubora wa
viwango vya Afrika vinavyotolewa na Chama cha Netboli Afrika (AN).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Anna Bayi, alisema viwango hivyo  vinavyotolewa na IFNA, vinaifanya Tanzania kutambulika zaidi kimataifa katika mchezo wa netiboli.

"Viwango hivi vimetolewa na IFNA juzi, baada ya kuona uwezo wa Tanzania waliouonesha katika mashindano ya kimataifa yaliyofanyika nchini Singapore wiki iliyopita, na Tanzania kushika nafasi ya tatu, hivyo tuna imani timu yetu itaendelea kufanya vizuri katika mchezo huu na kuitambulisha zaidi Tanzania kimataifa," alisema.

Alisema sasa ni wakati wa wadau mbalimbali wa michezo nchini, kuisaidia timu hiyo ili iweze kushiriki mashindano mengi ya kimataifa yatakayoiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kushiriki Kombe la Dunia la netiboli hapo baadae.Mwenyekiti huyo alisema ni wakati wa serikali kuipa ruzuku hata kidogo CHANETA, ili iweze kuendesha shughuli za kichama vizuri yakiwemo maandalizi ya kutosha kwa timu ya taifa.

No comments:

Post a Comment