08 December 2010

MICHUANO YA KOMBE LA CHALENJI Ethiopia, Ivory Coast zatangulia nusu fainali

*Kili Stars, Z'bar Heroes vitani leo

Na Elizabeth Mayemba

TIMU za Ivory Coast na Ethiopia, zimekuwa za kwanza kutangulia katika nusu fainali ya michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea katika Uwanja wa Taifa, baada ya jana kupata ushindi kwenye mechi zao za
robo fainali.

Ethiopia ndiyo iliyokuwa ya kwanza kutinga hatua hiyo, baada ya kuifunga Zambia mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa saa 8 mchana.

Katika mechi hiyo, Ethiopia iliibana Zambia ambayo katika hatua ya makundi iliwafunga wenyeji Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' bao 1-0, na ilikuwa ikipewa nafasi ya kupenya hatua hiyo, ambayo hata hivyo ililazimika kufunga virago baada ya kipigo hicho.

Mechi hiyo ilianza kwa kasi na Ethiopia, ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao ambalo lilitumbukizwa kimiani na Tesfaye Alebachew, dakika ya 18 baada ya kuunganisha krosi.

Bao la pili la Ethiopia lilifungwa na Omod Okwury, dakika ya 24 baada ya kupokea pasi ya Daniel Derebe. Zambia walipata bao la kufutia machozi dakika ya 58, bao ambalo liliwekwa kimiani na Felix Sunzu, baada ya kuwatoka mabeki wa Ethiopia.

Katika mchezo huo mchezaji wa Zambia Thomas Nyirenda, alizawadiwa kadi nyekundu dakika ya 36 baada ya kung'ang'ania mpira usipigwe faulo.

Nayo Ivory Coast ilijihakikisha kucheza nusu fainali, baada ya kuifunga Malawi bao 1-0 lilifungwa na Kipre Tchetche, dakika ya 80 kwa shuti kali lililokwenda moja kwa moja wavuni.Mechi hiyo ilianza kwa nguvu, ambapo Malawi kama wangekuwa makini wangeweza kutoka na ushindi baada ya kupata nafasi nyingi, lakini hata hivyo wakashindwa kuzitumia.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu, huku kila moja ikitaka kupata bao la ushindi, lakini hata hivyo bahati iliangukia kwa Ivory Coast, ambayo ilifanikiwa kutumbukiza mpira wavuni na kuwafanya kutinga nusu fainali.

Kivumbi cha michuano hiyo katika mechi za robo fainali, kinatarajia kuendelea leo, ambapo wenyeji 'Kilimanjaro Stars' watakumbana na Rwanda saa 10 jioni wakati Zanzibar 'Zanzibar Heroes', itavaana na mabingwa watetezi Uganda saa 8 mchana. Mechi zote zitapigwa Uwanja wa Taifa.

No comments:

Post a Comment