15 December 2010

Katiba mpya Tanzania sasa haikwepeki-Tendwa

Na Tumaini Makene

WAKATI madai ya kuwepo kwa haja ya Tanzania kuwa na katiba mpya yakizidi kushika kasi kila kukicha kutoka kwa watu na makundi mbalimbali ndani ya jamii nchini, Msajili wa Vyama vya Siasa, Bw. John Tendwa naye ameweka bayana kuwa suala hilo
sasa halikwepeki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, mara baada ya kufungua mjadala uliokuwa na mada isemayo 'Je kuna umuhimu wa kuangalia upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano?" ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia (TCD), Bw. Tendwa alisema "lini tutaanza kuongea ukweli...tusidanganyane kuwa hatuna matatizo...kwa nini tuseme mfalme yuko sawa wakati hajavaa nguo...hili halina ubishi...lakini liweje."

Bw. Tendwa ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema kuwa madai ya katiba mpya isiyokuwa na ladha ya chama kimoja, ni kilio cha wadau wa demokrasia vikiwemo vyama vya siasa kwa muda mrefu sasa, tangu wakati ukiundwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Alisema kinachotakiwa sasa ni kwa wadau hao ni kuyawasilisha madai hayo katika mfumo unaotakiwa ili yachukue mkondo wa kisheria, mathalani vyama vya siasa kulifikisha katika Baraza la Vyama ambalo linatambulika kisheria na serikali, ili yafanyiwe kazi.

"Watu wanataka mabadiliko ya katiba...ni kilio cha muda mrefu cha vyama vya siasa, kilianzia katika 'pressure groups' miaka ya tisini hata wakati tunaanza mfumo wa vyama vingi tayari kulikuwa na kilio cha watu kutaka katiba mpya isiyokuwa na ladha ya chama kimoja, karibu miaka 20 sasa kilio hiki kipo."Wenzetu Kenya wamekuwa na tatizo hilo la kuwa na msukumo wa katiba mpya...sisi pia tuna matatizo mengi katika nyanja nyingi, tusidanganyane kuwa hatuna matatizo...kama mmemsoma jana Jaji Kisanga nami ningependa kumnukuu alisema kuwa Serikali inapaswa kusikiliza kilio hiki cha wananchi isipofanya hivyo itajuta baadae.

"Hapa leo tuna-brainstorm (kujadili) tu, hakuna ubishi wa hilo, lakini liweje, huu si ndiyo wakati wake sasa...lakini hawa wanapaswa kulipeleka katika Baraza la Ushauri la Vyama vya Siasa ambalo ndilo litapeleka serikalini kisheria...suala hili likija officially (rasmi) lina mkondo wake," alisema Bw. Tendwa.

Naye Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye alikuwa mwenyekiti wa mjadala huo kwa niaba ya Bw. Freeman Mbowe, alisema kuwa upo umuhimu sasa wa taifa kuwa na katiba iliyotokana na mapendekezo ya watu, ikiwa na misingi imara inayokubalika katika jamii nzima kwa mustakabali wa nchi yao.

Alisema kuwa katiba ya sasa iliandikwa 'kwa haraka haraka na kikundi cha watu wachache waliopewa kazi hiyo baada ya kuonekana wamefanya kazi nyingine vizuri ya kuunganisha vyama vya TANU na ASP, ili kupata Chama Cha Mapinduzi, ambapo katiba hiyo ilitumika kuweka hatamu za uongozi wa nchi ziliwekwa mikononi mwa chama hicho, badala ya kuwekwa kwa wananchi kupitia chombo kama vile bunge.

"Katiba hii iliyo na viraka karibu kumi na tano, ilikuwa katiba ya chama kushika hatamu za uongozi wa nchi, ambapo bunge halina mamlaka bali chama...Jaji Nyalali aliweka wazi mapema mapendekezo ya kuwa na katiba mpya, pendekezo hilo lilikataliwa, Jaji Kisanga pia katika tume yake ya White Paper, alieleza hilo, lakini likakataliwa.

"Tunataka katiba mpya inayotokana na mapendekezo ya watu, kwa kuwashirikisha wananchi, yenye misingi imara ya kidemokrasia kama vile masuala ya wagombea binafsi, haki za binadamu ziwekwe kisheria si jumla jumla tu," alisema Prof. Lipumba.Akiwasilisha mada ya uchokozi katika mjadala huo, mara baada ya kufunguliwa, Mwanasheria kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bw. Harlod Sungusia, alisema kuwa katiba ya sasa ina kasoro nyingi ambazo zinatia dosari nchi na kulifanya taifa kukosa dira ya wapi linaelekea.

"Nikianza mada yangu ya uchokozi kwa kumnukuu Rais Mstaafu Mkapa aliyesema hivi karibuni kuwa katiba ni moyo wa Taifa sawa na moyo katika mwili wa binadamu, sasa unaweza kujiuliza huu moyo wetu wa Taifa la Tanzania wenye viraka na matundu namna hii...maana yake Taifa litakuwa linaumwa sana kwa sababu moyo wake hauko sawa. Kama wagonjwa wa moyo wanapelekwa India kwa ajili ya upasuaji, taifa litapelekwa wapi kupasuliwa.

"Katiba hii ya mwaka 1977 iliyopo sasa pamoja na ubovu wake lakini bado imejaa viraka, mpaka sasa imefanyiwa marekebisho mara kumi na nne...ni katiba ambayo unashindwa kuelewa inamilikiwa na nani, maana wananchi hawakuwahi kushirikishwa katika mchakato wa kupatikana kwake...kwa uhakika katiba zote kuanzia ile ya mwaka 1961, 1992, 1964, 1965 na hii ya sasa ya mwaka 1977 wananchi hawajawahi kushirikishwa.

Huku akiweka bayana matatizo mengi yaliyoko katika ibara na vifungu, aliainisha maeneo kadhaa yanayotia kasoro katiba ya sasa kuwa ni pamoja na historia ya mchakato wake, umiliki, kutoweka bayana utaratibu wa kuibadilisha, uhusiano wake (hadhi yake) dhidi ya sheria zingine, uhusiano wake na Katiba ya Zanzibar na pia kutotoa dira ya taifa, ambapo bado inazungumza "Tanzania ni nchi ya kijamaa."Wakichangia katika mjadala huo, viongozi waandamizi wa vyama mbalimbali waliokuwepo, kila mmoja alionesha wazi umuhimu wa nchi kuwa na katiba mpya, huku wengine wakitoa mfano wa nchi ya Kenya, kuonya kuwa gharama za kutokuwa nayo zinaweza kuwa kubwa zaidi, zikiligharimu taifa.

Bw. John Cheyo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha United Democtratic Party (UDP), alisema haja ya kuwa na katiba mpya i wazi, ambapo masuala mengi yanapaswa kufanyiwa kazi kama vile mfumo wa uchaguzi, kushirikisha wananchi katika utungaji "tunagalie upande wa pili wa shilingi, kutokuwa na katiba mpya gharama yake ni kubwa mno, hakuna jambo la kuogopa kudai katiba mpya, twende kwa wananchi kuwahamasisha wadai."

Naye Peter Mziray wa APPT-Maendeleo, alisema kuwa katiba iliyopo si wananchi, hivyo mchakato rasmi wa kudai mabadiliko ya wananchi uanze 'leo leo' kwa kukusanya majina ya ili papatikane mahali pa kuanzia.Bw. Benson Kigaila wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema kuwa kuna ulazima wa TCD, ambacho ni chombo kwa ajili ya vyama vyenye wabunge, kuitisha kongamano kuwahusisha wadau wengine zaidi ili kupanua wigo wa madai hayo ya muda mrefu.

Pamoja na mjadala huo kuhudhuriwa na vyama vya siasa mbalimbali, bado hoja ya kuwa na katiba mpya ilionekana kutawala kwa kila aliyeinuka kuzungumza ingawa kulikuwa na tofauti kadhaa za njia zipi zitumike kulisukuma jambo hilo kwenda hatua iliyopo sasa ya kudai katika makongamano na mijadala, kwa takribani miaka 20 sasa.

4 comments:

  1. BINAFSI NAMTIA RAIS JAKAYA KIKWETE MOYO WA IMANI ATOE TAMKO LA KUFANYIKA MJADALA WA KATIBA MPYA, AKITOA RATIBA NA MUDA MAALUM WA KAZI HIYO KIKAMILIKA. SIONI BUSARA YA RAIS KUKAA KIMYA NA KUWAPA CHADEMA, VIONGOZI WA ZAMANI (AMBAO HAWANA CHA KUPOTEZA), WASOMI NA WANANCHI KWA UJUMLA PEKEE WAKIWA MSTARI WA MBELE.HII ITAKULA KWA CCM NA SERIKALI YAKE.AIDHA NI KUWAWEKA VIONGOZI WALIOKO MADARAKANI KWENYE MTIHANI MGUMU KWA SABABU KAMA RAIS KAKAA KIMYA WEWE UNAANZIA WAPI. VIONGOZI WA AINA YA KINA TENDWA, JAJI RAMADHANI, SITTA, NK HAWAZALIWI KILA SIKU. BUSARA YA KIKWETE ITUNUSURU CCM, TENA NI SASA.

    ReplyDelete
  2. Ndugu Mhariri wa gazeti la Majira, nasikitika sana kuona kuwa watu wanaotoa maoni yao katika magazeti takribani yote wanakimbilia zile habari zenye "sukari au chumvi" za kisiasa tu. Nina maana kuwa masuala yanayokugusa jamii kwa mapoja hayapati maoni ya watu kwa wingi ila yale yanayogusa manufaa kwa wachache yanaonekana kupewa maoni kwa wingi. KWA HIYO MCHANGO WANGU KATIKA HABARI HII NI KWAMBA SUALA YA KATIBA MPYA SI OMBI NI LAZIMA SERIKALI IANZE KULIFANYIA KAZI SASA. WALIO MADARAKANI SASA WASIDHANI BAADA YA KUMALIZA MUDA WAO WA UONGOZI NDIO MWISHO WA DUNIA. WANAWEZA KUKUTWA NA MATUKIO MABAYA YANAYOHUSU UBOVU WA KATIBA HATA BAADA YA WAO KUJIUZULU UONGOZI.

    ReplyDelete
  3. pETRO eUSEBIUS mSELEWADecember 15, 2010 at 3:40 PM

    Mi nilidhani ile kasi mpya ingekuja na Katiba mpya.Sasa kasi zaidi,madai ya Katiba zaidi! Jamani,hili suala la Katiba mpya hili lisitufanye tusahau mambo mengine.Ninachokiomba ni sisi kuendelea na mambo mengine ya msingi kwakuwa viongozi wetu 'wasikivu' wameshasikia.Watasingizia kuwa mijadala ya Katiba imekula pesa na muda wa miaka mitano...muda si mrefu yaweza kuundwa Tume ya uchunguzi ya kuwepo kwa madai ya Katiba mpya!!!Kama vp tuwape deadline...wakishindwa tuchukue hatua.Vikishindikana vyote,tuhame.

    ReplyDelete
  4. HAKIKA NCHI YETU YA TZ INA MAMBO YA KUSHANGAZA KILA SIKU..HIVI TENDWA AMEJIFUNZIA WAPI NA SHULE IPI INAYOTOA SHAHADA ZA UNAFIKI KAMA AMBAVYO ANAONSHA MR TENDWA? LEO ANAUNGA MKONO KUWEPO KWA KATIBA MPYA!!! NASHANGAA..MBONA ALISHALALAMIKIWA MUDA MREFU,HAKUCHUKUA HATUA WALA HAKUSEMA LOLOTE...KWASABABU CHADEMA WAMEANZISHA NA AMESHAGUNDUA KWAMBA WANANCHI WATAUNGA MKONO...NA RAIS WAKE AMESHAFANIKISHA LENGO..SASA ANAKUBALI KATIBA MPYA ILI WENZAKE WAKWAE KISIKI..HATA KIKWETE ATAKUBALI MUDA SI MREFU ILI MGOMBEA WA CCM ANAYEKUJA AJIKWAE.

    ReplyDelete