02 December 2010

Polisi watakaoshindwa wajibu waondoke-Nahodha

Na Eckland Mwaffisi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha amewataka askari wote wa Jeshi la Polisi ambao watashindwa kusimamia haki na wajibu wa kazi yao kutafuta kazi nyingine ya kufanya ili kulinda heshma ya jeshi hilo kwa raia na nchi kwa
ujumla.

Bw. Nahodha aliyasema hayo Dar es Salaam jana, ikiwa ni siku ya kwanza kazini, wakati akizungumza na wakuu wa idara na vitengo mbalimbali vilivyopo chini ya Wizara hiyo.

Akionesha kufurahishwa na uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuwa msimamizi wa wizara hiyo, Bw. Nahodha alisema, ndoto yake ya muda mrefu tangu aanze kazi serikalini ni kusimamia haki za watu, amani, usalama wa raia na mali zao.

Alisema pamoja na changamoto nyingi walizonazo watumishi wa wizara hiyo, wajibu wa kila askari ni kusimamia haki kwa raia wote badala ya kutanguliza maslahi binafsi ambayo ni kinyume na mwongozo wa kazi hiyo.

“Sitavumilia utendaji kazi wa mazoea ambao ni kinyume na maadili ya utumishi serikalini, nimepata nafasi hii katika umri mdogo ambao sihitaji kulala sana, nitatumia muda mwingi kuwatumikia wananchi, kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika kuzitatua,” alisema Bw. Nahodha.

Aliongeza kuwa ili kulinda heshma ya Jeshi la Polisi na idara nyingine zilizopo chini ya wizara hiyo, miezi sita kuanzia sasa atahakikisha kasoro zote zinazoendelea kujitokeza zinafikia kikomo, kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumishi na huduma kwa raia ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wote.

Bw. Nahodha alisema dhamira yake ni kubadilisha utaratibu uliopo kwa kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa wizara ili uendane na matakwa ya wananchi.

“Nitazungumza pale wanapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo lakini kubwa na la msingi, nitafanya kazi kwa vitendo zaidi, nataka wizara yangu isifike kwa mazuri au ihukumiwe kwa mabaya katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa,” alisema.

Aliwataka watumishi wa wizara hiyo na Maofisa wa Jeshi la Polisi, kutekeleza wajibu wao bila kubagua watu wa kipato cha chini au cha juu bali kila raia, anastahili kupatiwa huduma inayostahili.

Waandishi waliohudhuria mkutano huo, walitaka kufahamu sababu inayochangia kusuasua kutolewa kwa vitambulisho vya taifa ambapo Bw. Nahodha, alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Idara hiyo, Bw. Joseph Makani, kulitolea ufafanuzi.

“Ni kweli tumechelewa kutoa vitambulisho ila hatua tuliyofikia ni nzuri, Februari 8, 2011 tunatarajia kumpata mkandarasi na Agosti mwakani, vitambulisho hivi vitaanza kutoka kwa awamu ya kwanza,” alisema Bw. Makani.

Bw. Nahodha ambaye alionekana kutoridhika sana na jibu hilo, alimwagiza Bw. Makani na timu yake wakutane leo asubuhi ili kuzungumzia jambo hilo na kusisitiza kuwa, mazungumzo hayo yataleta matumaini ya vitambulisho hivyo kupatikana mapema zaidi.

Pia Bw. Nahodha alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema wakutane kesho mchana ili aweze kumpa mikakati ya jeshi hilo katika kupambana na vitendo vya uhalifu ambavyo vimeibuka kwa kasi hasa mkoani Kigoma.

Aliongeza kuwa serikali inashughulikia madai ya watumishi wa wizara hiyo katika idara mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa kazi na kuwataka wakuu wa idara hizo, kuhakikisha watumishi wao wanapata fursa za kwenda kusoma ili kuongeza maarifa.

“Naamini watendaji nilionao wana uwezo mkubwa kiutendaji, nitashirikiana nao na kupokea mawazo yao ili kuboresha ufanisi wa huduma tunazotoa kwa wananchi,” alisema.

Bw. Nahodha aliahidi kukaa na uongozi wa Jeshi la Magereza nchini na Mkuu wa Idara ya Uhamiaji ili kulipatia ufumbuzi wa haraka tatizo la msongamano wa wafungwa magerezani na wahamiaji haramu.

4 comments:

  1. Nilitegemea waziri aliye serious angeanza na suala la maslahi ya askari magereza na polisi ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia katika ukiukwaji wa maadili,vipi askari anayekesha akipambana na wahalifu na ambaye maisha yake kila dakika ameyaweka rehani umlipe mshahara wa laki na nusu ambazo hazitoshi kabisa kukidhi mahitaji yake na sio proportion na risk atttached to his duties.Kuna mabo mengi ya msingi inabidi ayaangalie huyu waziri kabla ya kukimbilia vitisho kwa askari,
    -Suala la maslahi iwe priority number one,pia aangalie ukabila na udini katika promotion na posting,ili lilikanushwa lakini lipo.Ripoti ya Warioba ililipoti Rushwa kubwa within [yaani ya wao kwa wao ili pia aliangalie,mfano property nyingi alizonazo IGP mstaafu Mahita ni marejesho toka mikoani,kila RPC alikuwa anawajibika kumpelekea fedha ,mifugo,asali,mbao etc,kulingana na bidhaa zinazopatikana mkoani mwake,hii ilikuwa ni lazima kinyume na hapo hutadumu hata kama ni mtendaji mzuri,kwa Mwema nasikia hii kitu hakuna.Waziri mpya pia aangalie selection za watu wanaopelekwa Darfur na kwenye special operation nyingine atagundua madudu mengi sana.Kitengo cha fedha makao makuu kichunguzwe hapo ndipo kuna ufisadi wa kutisha,mapato na matumizi ya Osterbay mess yaangaliwe na mess nyingine nchini,kwanini mtu kama Chiko aliyekuwa na tuhuma lukuki za ufisadi na kujilimbikizia mali apewe usimamizi wa osterbay baada ya kustaafu ?hapo kuna kitu kimefichwa.
    -Zamani ajira ya polisi mtu alikuwa anaichagua akiwa shuleni mara baada ya kumaliza mtihani na anachaguliwa kulingana na matokeo,hii ilfanya watu wenye wito wajiunge na kazi hiyo,sasa hivi system inayotumika ni kokoro,mtu anaamua kuingia polisi baada ya kuona kafeli mtihani,au kakaa mtaani muda bila kupata kazi,wengine wanakuwa tayari waliiisha kuwa vibaka,malaya etc ipo mifano mingi ya watu kama hao ambao leo ni polisi,nafahamu wengi pia ambao wanaingia kwa kutumia vyeti vya ndugu zao au rafiki zao,system hii ni mbaya na inachangia kushuka maadili.
    -Kuna mambo mengi yanayoitaji utafiti otherwise waziri atatibu symptons na si ugonjwa,mfano kwa askari navyowajua ukianza kwa vitisho kama alivyofanya tayari wanajenga negativity na pia wanaona hakuna security ya employment hivyo badala ya kuogopa wanaanza kujiandaa na maisha endapo watapoteza kazi na hii unaelewa matokeo yake ni nini.Ili mtu awajibike kwanza mpe cofidency ya job security,pili maboresho ya maslahi,pia muhakikishie mikakati ya kumuandalia maisha baada ya ku retire.Jiulize waziri kama polisi muadilifu akistaafu anakuwa mlinzi wa rungu kwenye duka la muhindi yule aliyebaki kazini ata behave vipi.

    ReplyDelete
  2. Suala la National IDs limekuwa kiporo cha muda mrefu sana. Hakika priorities ambazo watanzania wangependa kufanyika,hili la vitambulisho haliepukiki...Project nzima inaonyesha jinsi watu serikalini wasivyo makini, wanafanya kazi kwa mazoea. Ni lini watu wataanza kuwa seroius katika mambo ya msingi yanayohusu taifa??Do we real need akina MAGUFULI kila mahali serikalini?PLEASE TUNAOMBA HILI LISHUGHULIKIWE KWA DHARURA........

    ReplyDelete
  3. inakuwaje mtu kupewa uwaziri wa mambo ya ndani
    wakati hajawahi kuwa hata askari ataweza vipi kuonngoza wizara hiyo?

    ReplyDelete
  4. Kigezo cha kuwa katika nafasi husika sio labda uliwahi kufanya kazi hapo mwanzo, mfano Bw. Nahoza hakuwa askari wala askari magereza ila unamjua elimu yake. Kuwa makini tafuta profile yake kwanza kisha uanze na comments Said

    ReplyDelete