02 December 2010

Dereva taksi apigwa risasi, aporwa gari

Na Rashid Mkwinda, Mafinga

DEREVA teksi aliyefahamika kwa jina la Nicolaus Mwaikambo(25) mkazi wa Kinyanambo mjini Mafinga ameuawa na watu wasiojulikana kwa kupigwa risasi katika shingo yake na kuweka jeraha lililotoboa shingo yake kumpora gari.Marehemu
ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T 353 AZC alikodiwa kati ya saa 2:00 na saa 3:30 usiku katika eneo ambalo
anaegesha gari lake, Njia Panda ya Mufindi karibu na Kituo cha Mafuta cha Total.

Watu wa karibu na marehemu walidai kuwa, watu watatu walifika katika kituo hicho na kuhitaji gari ya kukodi ambapo walimchukua marehemu ili awapeleke Ndolezi, nje kidogo ya mji wa Mafinga.

Msimamizi wa teksi hizo, Bw. Robert Matanila alisema kuwa aliachana na dereva huyo majira ya saa 2:00 usiku baada ya kuelezwa kuwa anakwenda kuegesha gari, lakini alipata taarifa asubuhi kuwa dereva huyo amekutwa amekufa akiwa na majeraha makubwa mwilini mwake.

Alisema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa umeburuzika kama dalili za mapigano baina ya wauaji hao na yeye ambapo mara ya kumuua mwili wake waliutumbukiza katika mto, karibu na barabara iendayo Ndolezi.

Majira ya saa 4:00 asubuhi polisi wakiwa katika gari aina ya Land Rover Defender walifika karibu na stendi kuu ya mabasi ya mjini Mafinga ambako marehemu
alikuwa akiegesha gari lake ambapo madereva hao waliutambua mwili wa marehemu.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Bw. Evarist Mangara alisema kuwa bado hajapata taarifa za tukio hilo na kwamba alikuwa anawasiliana na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga ili aweze kutolea ufafanuzi tukio hilo.

Aidha baadhi ya madereva teksi wa eneo hilo wameeleza wasiwasi wa maisha yao na kusema kuwa jeshi la polisi kupitia dhana ya polisi jamii na ulinzi shirikishi liwe
na mkakati maalumu wa kupambana na uhalifu na mauaji ya madereva teksi.

"Jeshi la polisi litusaidie katika hiliĆ¢€¦tunafanya kazi kwa hofu ya kuuawa," alisema Bw. Nico Luwago dereva teksi wa mjini Mafinga.

Tukio hilo mkoani Iringa ni la tatu kuanzia mwaka jana na katika wilaya ya Mufindi ni tukio la pili.

No comments:

Post a Comment