02 December 2010

Mimi si waziri mpole-Kawambwa

Na Peter Mwenda

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa amesema yeye si waziri mpole kwa sababu ya kutotema cheche kama wenzake, bali ni mkali kwa utendaji wake wa kimya kimya.Akizungumza na wakurugenzi na wakuu wa taasisi zilizo chini ya
wizara hiyo jana, Dkt. Kawambwa alisema staili anayoitumia kuongoza si kuzungumza kila wakati, bali kufanya kazi kwa ufanisi wenye lengo lenye mafanikio.

"Wananiambia Dkt. Kawambwa wewe ni mpole sana, lakini ukweli ni kuwa ukali katika utendaji kazi wowote unastahili umakini, kwa sababu ukali hauna njia moja, ipo ya kimya kimya ipo ya kusema sema," alisema Dkt. Kawambwa.

Alisema baada ya kuanza kazi ameweka vipaumbele katika mikopo ya wanafunzi, maslahi ya wafanyakazi na maboresho ya miundombinu ya majengo katika shule za msingi mpaka vyuo vikuu.

Dkt. Kawambwa alisema mikopo inahitaji kuongeza vyanzo vya kuongeza mikopo, hiyo ambayo kwa sasa ni asilimia 10 ya bajeti ya wizara hiyo, sawa na sh. bil. 200.

Alisema fedha hizo hazitoshi kwa wanafunzi ambao wanahitajika kupata mikopo badala ya wenye alama za daraja la kwanza na pili, iongezeke kama kwa madaktari na wataalamu wengine.

Alisema ili kulifanya taifa lipige hatua kiuchumi, wizara ya elimu inapaswa kuboresha mikopo hiyo hasa baada ya kamati ya kuchunguza mikopo ya wanafunzi iliyoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete itakapokamilisha kazi yake.

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi, alisema amejipanga kuboresha mishahara na pensheni kwa wastaafu wa wizara hiyo hasa walimu. "Ulikuwa Mwalimu pale Chuo Kikuu baada ya kustaafu unaonekana Kariakoo ukiwa umevaa kandambili zimetoboka," alisema Dkt. Kawambwa.

Dkt. Kawambwa alisema katika kuboresha mindombinu amejipanga kuongeza na kujenga majengo katika shule za msingi, Shule za Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu na kuongeza vitendea kazi na maktaba.

Alisema pia ameazimia kuboresha kiwango cha elimu kinachotolewa Tanzania kilingane na nchi nyingine duniani kutoka elimu ya awali, msingi, sekondari hadi vyuo vikuu.

"Roma haikujengwa kwa siku moja, tunatengeneza mitaala yetu iendane na mahitaji yetu ya Tanzania. Nchi ya Singapore wahandisi wake ni Wasingapore, tunataka wataalamu wetu wenyewe," alisema Dtk. Kawambwa.

Alisema Wachina hawana kawaida ya kupiga kelele wanapofanya kazi, lakini matokeo ya kazi zao hayalinganishwi na nchi nyingine na kutoa mfano wa reli ya kasi zaidi iliyoundwa nchini humo kuwa haijawahi kutengenezwa nchi nyingine duniani.

Awali, wakati Dkt. Kawambwa akitambulisha wakurugenzi hiyo alijisahau na kutaja wizara hiyo kuwa ya Miundombinu ambayo alikuwa anaoingoza kabla ya kuteuliwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuamsha vicheko kutoka kwa watu waliokuwemo.

"Mazoea yana tabu, bado nakumbuka Wizara ya Miundombinu," alisema Dkt. Kawambwa na kusema hiyo ni wizara yake ya tano baada ya Mifugo, Maji, Mawasiliano, Miundombinu na sasa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

3 comments:

  1. Namwoba Kawambwa aweze kufanya mabdadiliko na kuhakikisha madai ya waalimu na watumishi wanaofanya katika wizara hiyo yashuhulikiwe na kuondoa matatizo hayo,

    ReplyDelete
  2. Mheshimiwa Kawambwa,usitudanganye ulipokuwa miundo mbinu ulishindwa kujenga bara bara ya manyoni Singida.Na isitoshe mgogoro wa wafanyakazi wa railway na kampuni ya Right ya India.Mheshimiwa Kawambwa ninaomba ubadilike uache kuendekeza undugu wako na Mh.Jakaya Kikwete

    ReplyDelete
  3. Walimu wanamaliza vyuo vikuu wanalipwa pesa inayowafanya waikimbie kazi hiyo.Tunamaliza darasa moja mwingine akipata kazi sehemu nyingine analipwa mara tatu ya wewe uliyebaki katika kazi ya ualimu.Msipoangalia upya maslahi ya walimu, mtawafundisha kila mwaka lakini wanaobaki katika kazi hiyo ni moja ya tano tu. Mwalimu unakuwa na masters, hupandi daraja wala na mshahara unaongezeka kidogo tu nani atabaki kufundisha serekalini?Dr. kawambwa naomba uangalie muundo wa wizara na wasomi waliopo katika wizara hii wanahudumiwa vipi?karibu Elimu

    ReplyDelete