17 December 2010

Pinda awataka Mwaziri kusimamia haki za mtoto

Na Glory Mhiliwa, Arusha

MAWAZIRI wa nchi za Maziwa Makuu wenye dhamana ya  kuongoza Wizara za Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto wametakiwa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu haki za wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji, unyanyapaa  na
ubaguzi.

Hayo yalielezwa jana na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda wakati alipokuwa akifungua mkutano wa tatu wa mawaziri wa maendeleo ya jamii jinsia na watoto kutoka nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Bw. Pinda alisema kuwa kwa zaidi ya muongo wa karne moja nchi za Afrika zikiwemo za Maziwa Makuu zimekuwa na migogoro na vita hatua ambayo imesababisha  kundi la wanawake na watoto kuathirika zaidi kuliko makundi mengine hivyo ni wakati wa kuhakikisha wanawake na watoto wanakuwa kwenye hali ya usalama.

"Huu ni wakati sasa wa kutenda si wakati wa kupanga maana huu ni mkutano wenu wa tatu wa kwanza mliufanyia  Kongo  wapili  mwaka jana ulifanyika Mombasa Kenya mikutano yote mlikuwa mkiweka mikakati sasa ni wakati wa kutekeleza hiyo mikakati siyo kuendelea kuweka mikakati tena," alisema Bw. Pinda.

Alibainisha kuwa pia ni muhimu kundi la wanawake kama ilivyo kwa makundi mengine ya kijamii yakapatiwa nafasi sawa katika upande wa kijamii kama nafasi za uongozi na elimu ili kuhakikisha kuwa nao wanashiriki katika harakati za kijamii kiuchumi na kimaendeleo badala yakuwa watazamaji.

Aidha mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kufungua mkutano huo Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto hapa nchini, Bi. Sophia Simba alisema kuwa Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za maziwa makuu zimekuwa mstari wa kwanza katika kuhakikishakuwa haki ya mwanamke inalindwa na kuthaminiwa.

Alisema kuwa umoja wa nchi za Maziwa Makuu kwa  kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) na Taasisi ya kimataifa ya mfuko wa maendeleo ya wanawake [UNIFEM] wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mwanamke na mtoto wa nchi  za Maziwa Makuu anaishi kwa amani bila bughudha anaheshimiwa analindwa na kuthaminika sambamba na kushirikishwa katika mustakabali wa maendeleo ya nchi yake.

No comments:

Post a Comment