17 December 2010

Jaji Mkuu agoma kujitoa kesi ya 'samaki wa Magufuli'

Na Grace Michael

JAJI Mkuu wa Tanzania Augustino Ramadhan amegoma kujitoa katika usikilizaji wa rufaa iliyowasilishwa na washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi haramu ya kutaka marejeo ya uamuzi wa dhamana uliotolewa na Mahakama Kuu ya
Tanzania.

Hali hiyo ilijitokeza jana katika Mahakama ya Rufaa Tanzania ambapo upande wa Jamhuri uliwasilisha hoja ya awali ukimuomba Jaji Mkuu kujitoa kusikiliza rufani hiyo kutokana na misimamo yake ambayo amekuwa akiitoa katika nyakati mbalimbali.

"Kabla hatujaendelea na kesi, tunaomba tusikilizwe jambo la awali...hoja yetu n kwamba Jaji Mkuu ambaye ni mmoja wa Jopo amewahi kutoa maelezo mbalimbali kuhusu kesi hii akionesha msimamo wake na moja ya eneo ni mkoani Arusha kwenye mkutano wa majaji lakini pia aliwahi kunukuliwa na magazeti akizungumzia kesi hii hivyo tunaona ni vyema akajitoa kusikiliza kesi hii," alisema Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Stanslaus Boniface.

Alizidi kueleza kuwa pamoja na kesi iliyopo mahakamani hapo inalenga masuala ya dhamana lakini hata hicho kipengele nacho Jaji Mkuu aliwahi kukizungumzia akidai kuwa washtakiwa hao walishakataliwa dhamana hivyo akasema kuwa inaonesha moja moja kwa moja msimamo wake katika kesi hiyo ambayo anasema hawakustahili kushtakiwa washitakiwa wote hao.

Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, upande wa washitakiwa ambao uliwakilishwa na Bw. John Mapinduzi uliiomba mahakama kuendelea na kesi kwa kuwa hoja zilizowasilishwa hazikuwa na msingi wowote.

"Hoja hazina msingi kwa kuwa tangu huo msimamo utolewa Mei mwaka huu hakuna mtu yoyote aliyeingilia kati na kutoa dhamana na endapo hotuba hiyo ilitolewa mbele ya majaji wote basi hakuna jaji atakayeweza kusikiliza kesi hii ambayo washitakiwa wake wanazidi kuteseka rumande na mwingine alishapoteza maisha yake akiwa gerezani," alisema Bw. Mapinduzi.

Hoja hiyo pia ilizidi kupingwa na upande wa Serikali ambao walisema kuwa aliyeonesha msimamo wa wazi ni Jaji Mkuu na sio majaji wengine hivyo majaji wengine wanaweza kusikiliza kesi hiyo.

Hata hivyo baada ya malumbano hayo badala ya kutolewa uamuzi wa kujitoa au la, Jaji Mkuu aliamuru kuendelea kusikilizwa kwa rufani hiyo na uamuzi akasema atautoa kwenye hukumu ya rufani hiyo.

Baada ya kutoa amri hiyo, wakili wa washitakiwa Bw. Mapinduzi alianza kueleza kuwa rufaa yao inaiomba mahakama kurejea masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama Septemba 11, mwaka jana yakiwataka washtakiwa kuweka mahakamani sh. bilioni moja ambayo ni nusu ya gharama za samaki walizokamatwa nazo washitakiwa.

Alisema kuwa mashtaka yaliyotolewa uamuzi ni tofauti na mashtaka yanayowakabili kwa sasa ambayo hayana gharama yoyote kama yalivyokuwa ya mwanzo ambayo yalionesha samaki wa thamani ya sh. bilioni mbili.Mbali na hayo pia alisema kuwa masharti hayo hayakuzingatia sheria kwa kuwa idadi yao haikuzingatia kwa maana ya kugawana gharama iliyokuwa imetolewa hivyo akaomba mahakama kurejea uamuzi huo.

Hata hivyo Jaji Mkuu aliwataka kutoa maelezo yao haraka kwa kuwa alikuwa na safari ya Zanzibar kwa ajili ya kwenda kusikiliza kesi nyingine.

Baada ya kueleza hayo na upande wa mashtaka kujibu, Mahakama ilisema itatoa hukumu yake na kuzipatia pande zote mbili.

3 comments:

  1. JAJI MKUU INAKUBIDI UJITOE KWANI ULISHATOA MSIMAMO WAKO WAZI JUU YA SWALA HILI KWAHIYO NI WAZI UTAKUWA BIAS KTK KUTOA HUKUMU. NI AIBU KWAKO KAMA MSIMAMZI MKUU WA SHERIA KUWA MVURUGAJI WA SHERIA KWA JAMBO AMBALO LIKO WAZI NA SI KWA TZN TU BALI NI DUNIA NZIMA. FANYA HARAKA JITOE KUHESHIMU SHERIA.

    ReplyDelete
  2. Ni kweli serikali ilichemsha kuwaweka wachina wote ndani badala ya Kepteni. Hivi hakuna anayejua sheria za bahari huko wizarani?

    ReplyDelete
  3. Jaji Mkuu hana haja ya kujitoa hayo ni mazila yanayowapata Watanzania wengi tu hapa nchini,unaswekwa ndani miaka halafu unakuja kuondolewa ati huna hatia,tayari umeshateseka,huyo mtoa maoni wa kwanza hajatafakari maswali aliyoulizwa huyo mwendesha mashtaka na jaji mkuu,laiti angesoma angeelewa point za Jaji Mkuu,Jaji Mkuu atakuwa na maslahi gani kwenye upuuzi huo.Hawa watu wamekamatwa live kabisa hapo kuna uchunguzi gani haujakamilika zaidi ya DEAL YA MAWAKILI,WENDESHA MASHITAKA NA MAHAKIMU. NI UPUUZI KUSEMA JAJI MKUU ANA MASLAHI HAPO.JAJI MKUU/SERIKALI NI BORA UMFUKUZE KAZI HUYO MWENDESHA MASHTAKA KWANI KASHINDWA KAZI

    ReplyDelete