27 December 2010

Othman Chande jaji mkuu

Na Grace Michael

RAIS Jakaya Kikwete amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mohamed Chande Othman kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kushika nafasi inayoachwa wazi na Jaji Augustino Ramadhan anayestaafu.Jaji Ramadhan anastafu kwa mujibu wa
sheria kuanzia leo na nafasi yake inachukuliwa na Jaji Othman ambapo anatarajiwa kuapishwa leo katika viwanja vya ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ikulu jana, Jaji Othman mbali na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa pia ni mtaalamu binafsi juu ya hali ya Haki za Binadamu Kusini mwa Sudan.

Jaji Othman ambaye alizaliwa Januari Mosi, 1952 ana shahada ya kwanza ya Sheria (LLB) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili (MA) kutoka Chuo Kikuu cha Webster, Geneva, Uswisi.

Aliwahi kuwa Makamu wa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa inayosikiliza kesi za mauaji ya Rwanda, mjini Arusha na amewahi kushika nafasi sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huko Timor Mashariki.

Taarifa hiyo pia ilimwelezea Jaji Othman kuwa waliwahi pia kufanya kazi ndani na nje ya nchi katika Mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kama vile Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Oktoba mwaka huu, Jaji Chande aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa mwenyekiti mpya wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA).
                       
Akizungumzia uteuzi huo, Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria (TLS), Bw. Ibrahimu Bendra alisema kuwa uteuzi huo ni mzuri kwa kuwa Jaji Othman ana uzoefu mkubwa wa kimataifa.

“Kwanza niseme tu kwamba, haya maoni natoa mimi kama mimi kwa kuwa kama chama hatujakutana na ndio kwanza wewe unanipa taarifa hizi, lakini sina shaka yoyote na Jaji Othman, ni imani yangu ataleta changamoto kubwa ndani ya Idara ya Mahakama,” alisema Bw. Bendera.

Juzi wakati akiagwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jaji Ramadhan alieleza bayana kuwa upo mgawanyiko mkubwa ndani ya mhimili huo ambao unaweza ukawa na athari katika utoaji wa haki kwa Watanzania.

Jaji Ramadhan alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa kuna madudu mengi yanatofanywa kwenye Mahakama ya Rufaa ambapo katika kipindi chake aliwahi kuingilia hukumu mbili ambazo aliziona zimetolewa isivyo halali.

Lakini pia alikumbusha tukio lililotokea katika mkutano uliowakutanisha majaji wote, ambapo Jaji wa Mahakama Kuu na wa Mahakama ya Rufaa walizusha mtafaruku, hatua iliyosababisha kurushiana maneno, hivyo akasisitiza kuwa anayechukua nafasi hiyo anatakiwa kuwa mfano kwa majaji wengine wote.

1 comment:

  1. Nilifikiri JK kaacha udini? Kumbe mwendo mdundo

    ReplyDelete