08 December 2010

Neema nyingine yaingukia Chalenji

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom, imejitosa kudhamini mashindano ya Kombe la Chalenji yanayoendelea kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kutoa sh. milioni 190, ili kuongeza hamasa kwa mashabiki.Mashindano hayo pia yanadhaminiwa na
Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki (EABL), kupitia bia yake ya Tusker ambayo imetenga sh. milioni 650 kwa ajili ya kuendeshea mashindano hayo.

Akizungumza kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya fedha hizo, Meneja Udhamini wa kampuni hiyo, George Rwehumbiza alisema wanashukuru kwa kupewa fursa hiyo ya kudhamini mashindano hayo na lengo lao kubwa ni kuongeza nguvu kwenye michuano hiyo.

"Tumeamua kutoa sh. milioni 190, ili kuendeleza na kukuza soka la Tanzania na nina imani mashabiki watazidi kuongezeka katika mashindano haya kwa ajili ya kuhakikisha timu zetu za Tanzania bara na Zanzibar, zinalibakisha kombe nyumbani," alisema Rwehumbiza.

Naye Rais wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga aliishukuru kampuni hiyo kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu na anaomba wadhamini zaidi wajitokeze.

"Awali tulikuwa na upungufu wa fedha za kuendesha mashindano hayo na ndiyo maana tukaomba wadau wajitokeze zaidi, Tusker wakatoa sh. milioni 650 na baadaye tukapata sh. milioni 50 kutoka kwa wadau wengine," alisema Tenga.

Alisema baada ya kupata fedha hizo, bado walikuwa na deni kubwa kutokana na bajeti ya mashindano hayo ambayo ni sh, bilioni 1.5, hivyo fedha hizo walizopata kwa kiasi fulani zimepunguza deni hilo.

Tenga alisema kutokana na deni hilo kupungua kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana hata viingilio wamepunguza na cha juu kuwa sh. 5,000, badala ya sh. 10,000 kama ilivyotangazwa awali.

Alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), nia yake kubwa ni kufanikisha mashindano na si kutengeneza fedha kama baadhi ya watu wanavyowafikiria na kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, John Nchini kwa jitihada zake za kufanikisha udhamini huo.

No comments:

Post a Comment