08 December 2010

Taifa Queens yaanza vibaya Singapore

Na Amina Athumani

TIMU ya taifa ya Tanzania ya netiboli 'Taifa Queens', imeanza vibaya michuano ya Kimataifa inayofanyika Singapore baada ya kufungwa 46-33 na Scotland.Akizungumza kwa simu jana akiwa nchini humo, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Simone Mackinis alisema
Taifa Queens ilicheza kwa kiwango kikubwa isipokuwa ilizidiwa ujanja kipindi cha pili.

Alisema kipindi cha kwanza katika mchezo huo, Taifa Queens ilikuwa ikikaribiana na wapinzani wao kwa mabao kwani ilizidiwa kwa mabao mawili kwani hadi wanakwenda mapumziko Scotland ilikuwa ikiongoza 20-18.

Kocha huyo alisifia kiwango cha wachezaji wake walichokionesha katika mchezo huo ambapo Scotland, imewapa changamoto ya kufanya vyema katika mchezo unaofuata.Simone alipongeza kiwango kilichooneshwa na mchezaji Mwanaidi Hassan, ambaye ndiye aliyekuwa kinara wa kupachika mabao kwa upande wa Tanzania, kwani idadi kubwa ya magoli yalifungwa na mchezaji huyo.

Timu hiyo ya Tanzania itajitupa tena uwanjani leo asubuhi kwa kucheza na wenyeji Singapore na kesho itajitupa uwanjani kucheza na India.Michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kupata viwango vya kimataifa vinavyotambulika na Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (IFNA), ambao ndiyo wasimamizi mashindano hayo.

2 comments:

  1. Mpira wa pete ulikuwa na sifa kubwa enzi za kina Mbuke Tibanga ... sasa kwenye medani ya mpira wa pete Tanzania imekuwa kama kichwa cha mwendawazimu ...

    ReplyDelete
  2. Hebu tutafute mbinu tofauti za kuuboresha mchezo huu. Wakati huo tuwapunmzishe hawa Queens kucheza mashindano ya kimataifa ili kusubiri kuiva zaidi. Hii itatuondelea aibu kama hizi.

    ReplyDelete