16 December 2010

Mawasiliano hafifu kuzorotesha maendeleo Ukonga

Na Mwandishi wetu

MBUNGE wa  Jimbo la Ukonga Bi. Eugen Mwaiposa  amesema kuna mawasiliano hafifu baina ya watendaji na wenyeviti wa serikali za mitaa hivyo kuzorotesha maendeleo ya mitaa.Akizungumza jijini Dar es Salaam katika semina ya kukumbushana majukumu
iliyowakutanisha wenyeviti wa mitaa na madiwani katika jimbo la Ukonga

Bi. Mwaiposa alisema pia tatizo jingine linalokwamisha maendeleo ni bajeti zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya mitaa na Manispaa hiyo kutowashirikisha viongozi hao wa mtaa hivyo kutojua mradi waliyotengewa wala kiasi cha fedha kwa ajili ya maendeleo ya mtaa yao.

“ Wenyeviti hawashirikishwi na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ndio maana fedha nyingi zinatumika vibaya, kama wenyeviti wangeshirikishwa wangejua hujuma kwenye fedha hizi,” alisema     Bi. Mwaiposa.

Alisema kutokana na hali hiyo ni muhimu madiwani na Wenyeviti wa Mitaa kubadili mfumo wao wa utendaji kwa kushirikiana na kufuatilia kero zinazowakabili wananchi kuhakikisha wanazitatua kwa kushirikiana na wananchi hao.

“Tuhakikishe tunasimamia  miundombinu kwa kushirikiana na wananchi kama Barabara nyingi zipo hafifu za ndani ya mitaa ambazo ni jukumu la viongozi hao  kuzitengeneza,” alisema Bi. Mwaiposa.

Pia alisema Wenyeviti wa mitaa wahakikishe watoto wote waliofikia umri wa kuandikishwa darasa la kwanza wanaandikishwa bure wasitozwe fedha yeyote kwa kuwa watoto wanatakiwa wapate haki yao ya kusoma.

 “Si halali kumwacha mtoto asisome kwa ajili ya mchango wanatakiwa watoto wote wapate haki ya kusoma bure hivyo wenyeviti mnatakiwa kulisimamia hili tatizolililojitokeza kwa kila mtoto kuchangishwa Sh 30,000 ambayo si halali,” alisema Bi. Mwaiposa.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivule Majohe Bw. Hassan Kingalu amesema dampo la Pugu linaweza likasababisha mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuwa hizo taka hazigandamizwi na mashine na kumwagiwa mchanga ili  kuondoa harufu mbaya inayowakabili watu walio karibu na dampo hilo.

“Ilitakiwa magari yanapokuja kumwaga taka kulitakiwa kuwepo na Karandinga la kugandamiza taka halafu unamwaga mchanga kwa juu ili kuondoa harufu mbaya na kuepuka magonjwa ya kipindupindu ambayo yanayonyemelea katika eneo hilo”alisema Kingalu

"Dampo hili lilitakiwa liwe la kisasa matokeo yake limeletwa karandinga la kugandamiza taka ambalo liligharimu sh. 2  bilioni limefanya kazi wiki saba tu hiyo mashine imekufa na halifanyi kazi, ” alisema Bw. Kingalu.

No comments:

Post a Comment