16 December 2010

Jaji amuonya Manji kesi ya Mengi

Na Mwandishi Wetu

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania imemwonya mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam Bw. Yusuf Manji kuacha kuchelewesha usikilizaji wa kesi dhidi yake kwa kubadilisha mawakili kila inapopangwa kuanza kusikilizwa.Onyo hilo lilitolewa jana na Jaji wa
Mahakama hiyo, Bw. John Utamwa wakati akitoa uamuzi huo katika kesi ya kashfa iliyofunguliwa dhidi yake na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Bw. Reginald Mengi.

Uamuzi huo ulitokana na pingamizi lililowekwa na wakili wa mlalamikaji, Bw. Michael Ngalo aliyelalamikia ucheleweshwaji wa kesi hiyo ya mwaka 2006 na kudai umekuwa ukifanywa kwa makusudi na Bw. Manji kwa kuleta mawakili wapya kila shauri hilo linapokuja mahakamani kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Mbele ya mawakili wa pande zote mbili, huku Manji akiwakilishwa na mawakili watano, Jaji Utamwa alisema mara ya mwisho kesi hiyo iliahirishwa Oktoba 25 mwaka huu na kupangwa kuanza kusikilizwa Desemba 13 mwaka huu  lakini iliahirishwa tena baada ya jopo la mawakili wa Bw. Manji kutotokea mahakamani.

Badala yake siku hiyo, alifika wakili Cuthebert Tenga ambaye aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa madai kuwa Bw. Manji ameweka mawakili wapya na siku hiyo walikuwa na kesi zingine.

Jaji Utamwa alikubaliana na Bw. Ngalo kuwa utaratibu wa kubadilisha mawakili kila kesi hiyo inapokuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa unachelewesha mwenendo wa kesi na kuanzia sasa hatakubali tena hali hiyo ijitokeze.

Tangu kesi hiyo ipowasilishwa mahakamani hapo, baadhi ya mawakili waliojitokeza kutetea na baadaye kujitoa ni pamoja na  Rattansi, Theonist Rutashoborwa, Muganyizi, Jamal na baadaye alirejea tena Rattansi.

Jopo la mawakili linalomtetea sasa Bw. Manji katika kesi yake na Bw.  Mengi ni Bw. Yuda Tadey, Dkt. Ringo Tenga, Bw. Mabere Marando, Bw. Richard Rweyongeza, Tausi Abdallah na Bw. Cuthbert Tenga.

Baada ya kutoa uamuzi huo, jopo hilo la mawakili wa Bw. Manji ambalo jana liliongozwa na Bw. Marando, waliingia katika mzozo mwingine wa kutaka Wazee Baraza katika kesi hiyo, wajitoe. Hoja hiyo iliyosababisha kesi ya msingi isimame kwa takribani nusu saa, iliibuliwa na Bw. Marando akitaka wazee hao wa  Baraza, Bw. Ndimara Tegambwage, Bi. Rose Haji na Bw. Lugano Mbwina wasiwepo kwenye kesi hiyo kwa madai kuwa ni wana habari, hivyo wanaweza kuwa na mawasiliano na Bw. Mengi kwa vile ni mmiliki wa vyombo vya habari na pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT).

“Mheshimiwa Jaji, kwa kuwa sheria inayowapa nguvu Wazee wa Baraza kuwepo mahakamani imeshabadilishwa na kwa kuwa Bw. Mengi ni mmiliki wa vyombo vya habari na kiongozi wa MOAT na kwa kuwa wazee wote wa Baraza ni wanahabari kuna uwezekano wa wao kukutana na Bw. Mengi na kuathiri haki ya mteja wetu, hivyo wasiwepo kwenye kesi hiyo,” alidai Bw. Marando.

Hata hivyo Jaji Utamwa alitupilia mbali madai hayo na kutaka kesi hiyo ianze kusikilizwa. Shahidi wa kwanza kupanda kizimbani jana alikuwa Bw. Mengi ambaye alidai kuwa Bw. Manji alimkashifu na kumchafulia jina kupitia matangazo aliyoyatoa kwenye magazeti ya Tanzania Daima, Mtanzania, Tazama Tanzania na Majira.

Huku akihojiwa na Wakili Ngalo, Bw. Mengi alidai kuwa Manji kupitia matangazo hayo, alimwita mwongo, mzushi na kwamba amezoea kuzusha uongo kwamba anatishiwa maisha, kauli ambazo alidai zimemchafulia jina na kumuathiri  kisaikolijia.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Mengi amedai fidia ya mabilioni ya fedha. Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, imeahirishwa hadi Februari 15 mwakani.

3 comments:

  1. Hebu na hiyo kesi ianze imalize maana Mengi anahamu ya kuongeza umaarufu kwa kulumbana na kijana mdogo saizi ya mwanae! Yeye amekashifu wangapi? au mkuki wa guruwe tu?

    ReplyDelete
  2. OUVU NI OUVU TU HAWA MAFISADI WA KIHINDI NA JK WAO WAMEWAFANYAWATZ WAWE KAMA SWALA PORINI. HUYU MANJI SI NDIYE ALIINGIZA NSSF MNKENGE? NSSF NI SHIRIKA LETU, NANI ANAMTETEA FISADI KAMA HUYU KUWAKASHIFU WATZ WAZALEMNDO KAMA NAE HANA UBONGO WA KUFIKIRI?

    ReplyDelete
  3. mANJI ANAJULIKANA NI fisadi namba moja tanzania. Ni kweli kabisa kaka Manji anaifilisi nchi yetu huku watwala wakimbariki. Nasema hivi nguvu ya uma siku moja itafanya kazi na mafisadi wote tutawanyonga hadharani.

    ReplyDelete