LAS VEGAS, Marekani
BAADA ya kufanikiwa kutetea taji lake la uzani wa Light, bondia Juan Manuel Marquez amesema yupo tayari kuzipiga walau kwa raundi tatu na bondia machachari, Manny Pacquiao.Jumamosi iliyopita, Marquez alimsimamisha Michael Katsidis katika raundi ya tisa ya pambano hilo lililofanyika kwenye Ukumbi wa MGM Grand mjini Las Vegas na muda mfupi baadaye, akageuzia mawazo yake kwa kuelezea nia ya kupambana na Pacquiao ambaye anasemekana kuwa bora duniani.
“Kwa ujumla, Pacquiao ndiye ninayemtamani. Nitapandisha uzito na kufikia latiri 140, si tatizo,” Marquez alisema kupitia kwa mkalimani wake. “Manny acha kutoa sababu, pigana na mimi,” aliongeza.
Mabondia hao tayari walishakutana mara mbili siku za nyuma, ambapo katika pambano la kwanza la mwaka 2004 walipigana kwa raundi 12 na kutoka sare kabla ya Machi 2008, Pacquiao kushinda kwa pointi.
Promota wa Pacquiao, Bob Arum alisema katika mahojiano na Shirika la Habari la Marekani (AP), kuwa pambano la tatu dhidi ya Marquez linawezekana lakini bado wanangojea kuangalia kama, Floyd Mayweather Jr. atapanda ulingoni kuzipiga na Pacquiao katika pambano linaloonekana litakuwa na fedha katika historia ya masumbwi.
Mabondia wengine ambao tayari wanamtamani, Pacquiao ni pamoja na Shane Mosley ambaye tayari ameshaweka dau mezani na bingwa wa uzani wa welter, Andre Berto, aliyeshuhudiwa akidundwa katika raundi ya kwanza na Freddy Hernandez, wakati wa pambano la usiku ambao Marquez alitetea ubingwa wake.
No comments:
Post a Comment