Na Rehema Mohamed
RAIS Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa wapatao 3,563 katika siku ya maadhimisho ya miaka 49 ya Uhuru bila kuhusisha waliohusika na makosa ya kuwapa mimba watoto wa
shule wala waliowazuia kupata elimu.
Rais Kikwete alitoa msamaha huo jana kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Shamsi Vuai Nahodha ilibainisha kuwa, msamaha huo utawalenga wafungwa wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi jana walikuwa wametumikia robo ya vifungo vyao.
Wengine ni wenye magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu na saratani ambapo wanaelekea kuwa katika siku za mwisho za maisha yao baada ya kuthibitishwa na jopo la madaktari chini ya uwenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi watakaothibitishwa na jopo la Mganga Mkuu wa Mkoa au Wilaya, wafungwa wakike waliokuwa na mimba pamoja na walioingia gerezani na watoto wachanga wanaonyonya pia watahusishwa.
Wengine waliopata msamaha ni wafungwa walio na ulemavu wa mwili na akili ambao watathibitishwa na jopo la madaktari chini wa uwenyekiti wa Mganga mkuu wa Mkoa au Wilaya.
Taarifa hiyo ilibainisha kuwa msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, kifungo cha maisha wala wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Wengine wasiohusika na msamaha ni wale waliopatikana na makosa ya kupokea au kutoa rushwa, makosa ya ungang'anyi wa kutumia silaha, kupatikana na risasi au silaha, kunajisi, kubaka, kulawiti na wizi wa magari kwa kutumia silaha.
Wafungwa wengine ambao hawatahusishwa na msamaha huo ni wale waliohukumia kifungo kwa kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, waliotenda kosa hilo wakiwa na miaka 18, na kusababisha wanafunzi husika kushindwa kuendelea na masomo.
Wafungwa waliohukumiwa kwa makosa ya kuharibu miundombinu kama wizi wa nyaya za simu, umeme njia za reli na transifoma, walio na kifungo cha pili au zaidi, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa rais na wanaendelea kutumikia kifungo chao pia hawatahisishwa na msamaha huu.
Wengine wanotumikia kifungo chini ya sheria ya Bodi za Parole 1994 na sheria ya huduma kwa jamii 2002, waliowahi kutoroka au kujaribu kufanya hivyo chini ya ulinzi, waliopatikana na hatia ya kutumia vibaya madaraka na waliopatikana na hatia ya kuzuia watoto kupata masomo.
Mh.Rais hakutenda haki kwa wafungwa kifungo cha maisha.wafungwa wanaotumikia vifungo vya sio watanzania?au kwasababu hakuna mtoto wa kigogo aliefungwa maisha?Ninaomba Mh.Rais akumbuke kuwa nchi ya Tanzania inafuata utawala bora na sheria.Mh.Nahodha kwakuwa wewe ni katibu kwenye vikao vya msamaha kwa wafungwa ninaomba sana uwakumbuke wafungwa wa kifungo cha hususani waliokaa zaidi ya miaka15 na kuendelea.
ReplyDelete