16 December 2010

CUF yazinduka matokeo Uchaguzi Mkuu

*Yatuhumu Tume ya Uchaguzi kwa uchakachuaji
*Yataka Watanzania kuungana kudai katiba mpya
*Yavunja na kupanga upya safu yake ya juu

  
Na Tumaini Makene
ZIKIWA zimepita takribani wiki nne tangu kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompatia ushindi Rais Jakaya Kikwete, Chama cha
Wananchi (CUF) kimezinduka na kudai uchaguzi huo ulichakachuliwa na kwamba matokeo hayo yamepoteza imani ya Watanzania kwa Tume ya Uchaguzi (NEC) kwani haiwezi kusimamia uchaguzi huru na haki.

Chama hicho hicho pia baada ya kufanya tathmini ya kina ya Uchaguzi Mkuu na katika kujiimarisha ili kukabiliana na siasa za wakati uliopo pamoja na matokeo ya uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kimefanya mabadiliko makubwa katika nafasi zake kadhaa za juu, ikiwa ni pamoja na kuunganisha baadhi ya kurugenzi zake.

CUF kimesema kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame  imedhihirika wazi kuwa tume iliyopo haina sifa za kuweza kuaminika mbele ya macho ya Watanzania, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa tume huru na ya haki.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam juu ya maazimio ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa la CUF lililoketi siku  Novemba 10 hadi 11 mwaka huu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema;

"Baraza Kuu linawataka Watanzani wote wapenda demokrasia na mabadiliko kuungana pamoja kudai Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokuwa na misingi ya kidemokrasia ya kweli na itakayoweka Dira ya Maendeleo ya Taifa letu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na vijavyo. CUF inaungana na Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama au nafasi walizonazo katika jamii kwa kutumia njia za kidemokrasia kudai mabadiliko ya katiba mpya ili ikidhi matakwa ya wakati tulio nao.

"Sambamba na madai ya Katiba mpya, Baraza Kuu linawataka wadau mbalimbali na Watanzania wote kuendeleza madai ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi na haja ya kuwepo tume huru na ya haki ya uchaguzi wa nchi yetu, ambayo itaheshimika na kila Mtanzania kwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Kutokana na matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa...

"...na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imedhihirika wazi kuwa tume iliyopo haina sifa za kuweza kuaminika mbele ya macho ya Watanzania hasa ukizingatia kasoro, udanganyifu na mfumo wa uchakachuaji wa idadi ya wapiga kura waliojitokeza kuwa 8,626,283 kati ya wapiga kura 20,137,303 waliodaiwa kujiandikisha.

"Waliopiga kura 2010 ni sawa na asilimia 42.8 ya wale waliojiandikisha. Hii ni tofauti kubwa sana ukilinganisha na waliojitokeza kupiga kura 1995 (76.7%), 2000 (84.4%) na 2005 (72.4%). Watanzania wengi wamepoteza kabisa imani kuwa tume inaweza kusimamia uchaguzi ulio huru na wa haki.

Alisema kuwa Baraza Kuu  la chama hicho limempongeza Bw. Alassane Ouattara kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Cote d'Ivoire na linaungana na jumuiya ya kimataifa ikiongozwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani ubadilishaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo uliofanywa na Serikali ya Bw. Laurent Gbagbo.

Alisema Baraza hilo limesikitishwa na hatua hiyo ambayo inadhihirisha muendelezo wa serikali za nchi za Afrika kuvuruga uchaguzi na kutoheshimu maamuzi ya wananchi " CUF tunatoa mwito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa tamko la kumtambua Mheshimiwa Alassane Ouattara kuwa Rais halali wa Cote d'Ivoire,"alisema.

Akizungumzia mabadiliko ambayo ameyafanya kwa mujibu wa majukumu ya mwenyekiti yaliyoainishwa katika Katiba ya CUF, toleo la 2009 ibara ya 68 (1), Baraza Kuu limeidhinisha uwepo wa muundo mpya wa Kurugenzi za chama Taifa na kuthibitisha uteuzi wa manaibu katibu mkuu, wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wapya.

Alisema Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara ni Bw. Julius Mtatiro, kwa upande wa Zanzibar ni Bw. Ismail Jussa Ladhu, ambao kila mmoja kwa upande wake, pamoja na masuala mengine watasimamia pia majukumu ya Kurugenzi ya Utawala na Ulinzi wa chama.

Kurugenzi ya Uchumi na Fedha itakuwa chini ya Bw. Salum Mandari (Mkurugenzi) na Bi. Zakiya Omari Juma (Naibu). Kurugenzi ya Oganaizesheni, Uchaguzi Baraza la Wawakilishi na Bunge itaongozwa na Bw. Salim Hemed akisaidiwa na Bw. Shaweji Mketo.

Kwa upande wa Kurugenzi ya Haki za Binadamu, Uenezi na Habari, Bw. Salim Bimani atasaidiwa na Bi. Amina Mwidau, huku Bw. Faki Haji Makame akiteuliwa kuwa Mratibu Ofisi ya Katibu Mkuu, Seif Shariff Hamad, ambaye sasa amekuwa na majukumu mengi ya kiserikali akiwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Katika hatua nyingine pia, kwa mujibu wa Prof. Lipumba, Baraza hilo limewashukuru na kutoa pongezi maalum kwa wapiga kura wa Jimbo la Lindi Mjini kwa kumchagua Bw. Salum Barwany, ambaye ana ulemavu wa ngozi kuwa mbunge wao, kwa tiketi ya CUF. Alisema kuwa watu wa Lindi wameitoa kimasomaso Tanzania juu ya sifa hasi dhidi ya mauaji ya maalbino.

17 comments:

  1. Jina kama la Julius naona lipo moja tu katika orodha yote hiyo, Hongora Mtatiro wamegundua uwezo wako bila kujali dini yako.

    ReplyDelete
  2. Huo sasa uchokozi kenneth!

    ReplyDelete
  3. NAFURAHI CUF KUZINDUKA NA KUFUATA NYAYO ZA CHADEMA. TATIZO LA CUF NI KUJIONA WAO NI WAPINZANI WA CHADEMA NA SIO CCM. HAPO WALIKOSEA SANA. HATA BUNGENI CUF MJUE NDUGU YENI NI CHADEMA, NCCR NA TLP. THEN WA TZ WAKO NYUMA YENU NA MDAI KATIBA MPYA MTAPATA, ITS JUST A MATTER OF TIME. HONGERA CUF KWA HILI.

    ReplyDelete
  4. CUF NI WANAFIKI WATUPU HAWAPASWI KUONGEA KUHUSU UCHAGUZI MKUU. TUMEWAJUA NI NDUMILA KUWILI WENYE SUMU KALI SANA. TUSIPOANGALIA WANAWEZA HATA KUPINDISHA HUU MCHAKATO WA KATIBA MPYA. ENDELEEENI TU NA UNAFIKI WENU, YETU TUACHIENI.

    ReplyDelete
  5. ahhahaaaahaha Mtatiro kakomaa nao mpaka mwisho lakini kilichompata James Mapalapala nacho kiko njiani kwake...yaani CUF na udini wee acha tuu!!!!

    ReplyDelete
  6. Anonymous Said

    Wewe inaonesha unatumiliwa kueneza habari za udini ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF). Wewe ukue huwashi wala huzimi maana lugha hiyo imetumiliwa miaka na kina Vibaraka kama wewe kina Mapalala na wenziwe na hawakuweza kuiangusha CUF sembuse wewe karagosi

    CUF imara na ina malengo madhubuti ya kukongomboa nchi

    ReplyDelete
  7. Julius mtatiro alikosea alitakiwa ajiunge na chama lenye nguvu CHADEMA, aulize kilichomutoa Lwakatare CUF ni nini kama siyo baragashia

    CUf kwa sasa ni ccm b,

    ReplyDelete
  8. CUF si lolote si chochote ni uroho tu wa madaraka. Baada ya kuingizwa serikalini zanzibar sasa hamna tena meno mmekuwa kibogoyo. Chama cha kweli kikuu cha upinzani kitabaki kuwa CHADEMA. CHADEMA OYEEEEEE! PEOPLES POWER!

    ReplyDelete
  9. Nyinyi CUF mtaendelea kufagia ofisi za CCM mpaka mwisho na kuwapigia ukuta rangi wao wanaendelea kusaini vocha za pesa. Mmeshaajiriwa Zanzibar bado mnatafuta kibarua tena huku bara? Sasa kibarua cha huku bara kitakuwa ni nini? Endeleeni na taarabu zenu.

    ReplyDelete
  10. Ukisoma tu maoni mengi ya watowa maoni unapata picha hawa watu hawaijuwi CUF vizuri na wapi imeanzia.

    Ukianza na kesi ya mapalala. Wakati ule 1992 mpaka 1995, chama kilichowa kina sauti ni CUF, Licha ya NCCR kuwa nawasomi wengi. NCCR mageuzi walipata umaarufu kwasababu ya Mrema. Kilicho mfukuzisha Mapala si kwasababu ya dini yake. Ilikuwa ni tamaa yake ya pesa. na si yeye tu, wamepita wengi kama akina nyaruba. Mapalala kama mwenyekiti wa chama, alikuwa na mbinu ya kufuja ikikaribia wakati wa uchaguzi. Kilicho fuatia, CUF walikuwa wakisema, ikianguka sindano ikulu wao wanapata habari. Wakajulishwa habari zake. Kafukuzwa, cha ajaabu akawa kutwa yupo TVZ kuja kumwaga sumu na uongo mtupu na huku Zanzibar ndipo alipo hongwa hizo pesa. Wakafuatia akina nyaruba, na hapa mutasema hayo hayo kwasababu wakiristo. Nao wakafukuzwa hivyo hivyo. Lakini mumesahau tulikuwa na mwenyekiti mwengine Mageni Masobi ambaye mkiristo na alitokezea kupendwa sana na ilipofika wakati kutoka na afya yake na utu uzima, akaamua kujiuzulu na kubakia kama mshauri tu wa chama.

    Sasa tuje kwenye orodha ya Waislam kwenye CUF. Kuna Shaibu ambaye yupo Chadema sijuwi mpaka sasa au laa. Huyu ameondoka mwenyewe lakini ni muislamu. Kuna msabahaa. Kuna Fatma magimbi na othman hawa walipata fupa nono lakini hawakuweza kufanikiwa lengo lao la kutaka kukichafua chama. Kuna waasisi kama Khatib Hassan, huyu naye alitimulia kwa kikisaliti chama. Kwa hiyo tafuteni chengine cha kusema.

    Ya maridhiano na serikali ya umoja wa kitaifa, nyinyi sio munao kula pili pili na kujuwa inawasha vipi. hata yale maji ya kutawanya waandamanaji ya jeshi la polisi, hutumika kwetu Zanzibar tu nyinyi mukiwa shuwari. Sisi ndio kila ikifika uchaguzi, ndio tunao pigwa, kutungiwa kesi hewa, kufukuzwa makazini, kukosenywa hata haki zetu tukiwa nje ya Tanzania. Ukienda ubalozi wa Tanzania kubadilisha passport na wakijuwa unatoka Zanzibar, basi hupewi. Na msaada wowote ule hupati. Sasa hivi, alhamdullah tuna mshukuru Mwenyezi Mungu, tupo shuwari. Tumepat Raisjapo ni CCM na hatuna imani sana na CCM, lakini mpaka sasa ameonesha kuwa makini na amekuwa akitekeleza ahadi zote.

    ReplyDelete
  11. Hili ni rahisi sana kama CUF kuna udini Chadema kuna Kanisa na ndio nguvu yao yote inapigiwa debe na kanisa na kama utaangalia utaona yote hayo. Viongozi wa Makanisa ulikuwa huwasikii kuzungumzia suala la siasa TZ lakini baada ya kuona msimamo wa CUF ndio wameanza kuwa-support Chadema na kupiga kelele kuhusu Katiba baada ya Chadema kushindwa kwenye uchaguzi. CUF wameanza kudai katiba miaka mingi nyuma na angalia kumbukumbu kama ni mgeni wa siasa utaona. Tatizo kubwa la Chadema hawawezi kushirikana na vyama vyengine kwa sababu ya uroho wa madaraka na hili hatushangai kabisa kwa sababu ni kawaida yao lo wanamkandia Kikwete hadharani lakini kesho watakuwa ikulu wakitoa siri za vyama vyengine Chadema ni CCM B imeanzishwa kuua upinzani.

    ReplyDelete
  12. Nyinyi Anonymous# 3 & 6 inaonesha ni wabaguzi wakubwa wenye mrengo wa kikaburu. wacheni siasa za kibaguzi na mulete ushauri wenye kuboresha siasa za nchi na maendeleo ya wananchi.

    Suala la kidini na ukabila ni tools zilizotumika kwa makarne kuwagawa na kuwanyanyasa binaadamu.

    Article hii inahusu uboreshaji wa NEC ili chaguzi zinazofata ziwe za haki ambapo itarejesha imani ya wapiga kura

    Masuala ya udini, mavazi na uasili yametokea wapi.....

    ReplyDelete
  13. ACHENI UPUUZI NYINYI BAADA YA KUSAIDIA NCHI IENDELEE BADO HADI WAKATI HUU MNABISHANA KWA VYAMA CUF, CHADEMA,LIPUMBA MAPALALA U SEEM TO BE A CENTURY BACKWARD YATASAIDIA NINI HAYO?

    ReplyDelete
  14. CHADEMA, CCM NA CUF VINATAKIWA VIONDOE MLUNDIKANO WA WATU KUTOKA DINI MOJA AU KANDA MOJA;
    VYAMA VYOTE HIVI HAVIJAWAHI KUTAMKA HADHARANI KUBEBWA NA DINI FULANI LAKINI IMETOKEA WAMEKUWA NA SAFU YA JUU YA WATU WA DINI MOJA. INAWEZEKANA NI MAKUSUDI/KAMPENI YA SIRI AU HUJUMA.
    CCM UDINI UPO KILA MAHALI HATA UBALOZINI NJE YA NCHI. MADAI YA MAHAKAMA YA KADHI YALIKERA SAANA WAKRISTO NA UDINI WAKAUONA.
    CUF SAPOTAZ NDIO WANAOTAMKA UDINI LAKINI SI VIONGOZI. IMEJAA WAISLAMU WENGI KWAKUWA CHAMA HIKI KINAUNGWA MKONO SAANA NA WAZANZIBARI AMBAO WENGI WAO NI WAISLAMU.
    CHADEMA TATIZO SI UDINI BALI WATU WENGI WALIOKIUNGA MKONO TANGU AWALI NI KUTOKA K'NJARO, ARUSHA, MANYARA, MARA NA KIGOMA. HIVYO TUHUMA ZAO NI UKABILA NA UKANDA.
    HAWAT

    ReplyDelete
  15. siyo kweli! Chadema 1995 iliiunga mkono NCCR MAGEUZI, na mwaka 2000 iliisapoti CUF. Je, CUF imewahi kumsapoti nani?. 1995 mrema alikuwa na nguvu kuliko wagombea wote, CUF kwa sababu ya UDINI na tamaa ya MADARAKA wakasimamisha mgombea. 2000 lipumba alikuwa na nguvu, akapata sapoti ya DP na CHADEMA na 2005 alichuja na kukosa sapoti. 2010 Slaa alikuwa na nguvu kuliko LIPUMBA lakini Lipumba alikomaa kilinda maslahi ya chama chake, UDINI na ubinafsi. Anataka yeye tu tangu 1995, hasomi alama za nyakati kama wenzake akina mrema, mbowe na cheyo. SI AJABU 2015 tukaona Lipumba huyooo kutetea ubinafsi na udini.

    ReplyDelete
  16. Fundi mitambo wa Majira

    Hebu boresha mtandao wako kwa kuweka self generating Anonymous 'numbering' ili afahamike kwa ufasaha Anonymous aliechangia.

    Wakati mwengine tunataka kumsapoti au kumpinga Anonymous aliechangia lakini inakuwa tabu kumu-identify

    ReplyDelete
  17. KWELI KABISA KAKA YANGU LIPUMBA MBINAFSI SANA YAAANI KILA AWAMU ANATAKA AGOMBEE YEYE TU URAIS HUO NI UBINAFSI MKUBWA!!!

    ReplyDelete